November 25, 2016

ANGBAN

Na Saleh Ally
UONGOZI wa Klabu ya Simba umeanza kuyafanyia kazi masuala ya usajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara!

Simba wamemaliza mzunguko wa kwanza wakiwa wanaongoza kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya wapinzani wao Yanga ambao wako katika nafasi ya pili.

Taarifa zinasema Kocha Joseph Omog amesema anataka wachezaji watatu, kipa, beki wa kati na mshambuliaji mmoja wa kati ambaye atakuwa mpachika mabao. Sijajua kama kocha huyo atakuwa amesahau kusema kuhusiana na suala la kocha.

Wakati kocha huyo mtaalamu ameacha hilo, nimeshangazwa kuona atakuwa ameagiza kusajiliwa kwa kipa halafu akasahau kusema anahitajika kocha wa makipa wa kiwango sahihi.

Kocha wa makipa wa Simba, Adam Abdallah maarufu kama Meja, sijawahi kusema si kocha mwenye uwezo kwa kuwa nimewahi kumshuhudia akiifanya kazi yake vizuri. Lakini sitaacha kuendelea kusema kwamba kwa kiwango cha Simba, wanahitaji kocha zaidi yake.

Mfano, wako wanaolalamika kiwango cha kipa Vincent Angban raia wa Ivory Coast kilishuka katika hatua za mwishoni. Hakuna anayeona kuwa kuwa kipa huyo anaweza kuwa mzoefu au gwiji kuliko hata Meja.

Meja anahitaji kujiendeleza zaidi katika mambo ya kisasa zaidi katika nyanja hiyo ya makipa. Kwa kuwa mambo yanabadilika na unaona katika nchi zilizoendelea kisoka, ufundishwaji wa makipa unazidi kupiga hatua zaidi.

Kwa Simba ilipofikia sasa, inahitaji mtaalamu hasa katika nyanja hiyo ya upande wa makipa kwa kuwa ni sehemu namba moja katika ulinzi. Hata uwe na difensi bomba na wote mnakaba sana lakini kama mtakuwa na kipa ‘koti’ basi ujue ni tatizo.

MANYIKA

Tatizo la makocha wa makipa kutojiendeleza au Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoangalia kwa ukaribu kozi za muendelezo za makocha wa makipa kama sehemu ya kipaumbele, imekuwa ni tatizo kubwa sana katika mchezo wa soka nchini.

Makocha wa makipa wamesahaulika na wengi wamebaki kuwa na mbinu za kizamani na mara kadhaa nimekuwa nikisema hata Juma Kaseja kuonekana ameisha ilichagiwa na hili kwa kuwa hakuwa na mtu wa kumpa mbinu mpya ili aendelee kufanya vema au kukitia ‘ndimu’ kipaji chake kwa maana ya kukiboresha. Wanaomfundisha wengi hawakuwa na mbinu mpya.

Angalia Simba, walipata kipa bora wa makipa kwa ukanda wote wa Afrika Mashariki. Huyu ni Mkenya Iddi Salim ambaye aliondolewa pia baada ya kuondolewa kwa Kocha Dylan Kerr raia wa Uingereza.

Kama unakumbuka kipindi cha Mkenya huyo akiwa kocha wa makipa ndiyo kipindi Agban anaanza kurejea baada ya kutua nchini kiwango chake kikiwa kimeporomoka kutokana na kutokuwa amecheza kwa muda mrefu alianza kuwika taratibu.

Manyika alikuwa katika kiwango bora kabisa baada ya kocha huyo wa makipa aliyewahi kuinoa Gor Mahia ya Kenya na kuipa mafanikio makubwa kutokana na kuwa na makipa bora.

Iddi ndiye kocha aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuinua kipaji cha kipa Ivo Mapunda ambaye aliondoka hapa nyumbani akionekana ameisha, baadaye akawa shujaa na maarufu nchini Kenya.

Kocha huyo ambaye Simba iliamua kumuondoa huku ikiwa haina uhakika wa inachokifanya. Sasa inapiga hesabu za kusajili kipa bora jambo ambalo kwangu naona ni kichekesho kilichotolewa kwa makusudi kabisa.

Hata kama si Mkenya huyo, Simba inapaswa kutafuta kocha sahihi wa makipa ambaye atamsaidia Agban kuboresha kiwango, hali kadhalika Manyika ambaye akiimarika pia atarejea langoni afanye kazi yake.


Kusajili kipa mwingine sasa ni sawa na kuweka wazi kwamba Manyika hana nafasi na pia kutatua tatizo kwa muda tu halafu baadaye litakuwa palepale maana hata huyo bora atakayekuja, mwisho atahitaji huduma ya kocha bora na atakapoikosa, atarejea katika kiwango cha wale wanaoachwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV