Na Saleh Ally
CHELSEA sasa ipo kileleni mwa Ligi Kuu England ikiwa na tofauti ya pointi sita dhidi ya anayeshika nafasi ya pili, Liverpool inayonolewa na Kocha Mjerumani, Jurgen Klopp.
Vinara hao wana pointi 43 na Liverpool wana 37. Utaona tofauti ya pointi inazidi kuwa kubwa na Man City iliyo katika nafasi ya tatu na pointi 36, inafuatia Arsenal yenye 34.
Katika mechi 17 ilizocheza za ligi hiyo, Chelsea imepoteza mechi mbili tu, sawa na Liverpool na Tottenham iliyo katika nafasi ya tano na pointi 33.
Chelsea ina sare moja tu, ikiwa imefungwa mabao 11 ambayo ni machache zaidi lakini wastani wake wa kufunga si mkubwa sana kwani ina 35 ikiwa inazidiwa na Liverpool iliyofunga 41, Arsenal (38) na Man City (36).
Mwendo wa Chelsea unaonyesha ni timu inayokwenda kwa tahadhari kubwa, tena ambayo inaweza kwenda kwa ushindi wa kawaida lakini ikiangalia upatikanaji wa pointi tatu kwa umakini wa juu.
Hadi inacheza mechi 17, Chelsea imefungwa mabao 11 tu. Hii ni sehemu ya kuona kwamba, ugumu wa safu ya ulinzi ya Chelsea unaendelea kuwa silaha kubwa na huenda baada ya kufungwa mabao 3-0 na Arsenal, Chelsea imebadilika na uchezaji wake ni ule unaojali zaidi ulinzi kwa asilimia 90.
Ndiyo maana ni kitu cha kawaida kabisa kuona Chelsea inaendelea kushinda kwa bao 1-0 lakini ikiendelea kubaki kileleni. Unaweza kusema hii ni njia sahihi ya kupita ya Kocha Antonio Conte.
Ili ligi iishe, kila timu inatakiwa kuwa imecheza mechi 38. Tayari Chelsea imecheza 17, maana yake bado mechi mbili ili ikamilishe nusu ya safari ya Ligi Kuu England kwa msimu wa 2016-17.
Huwezi kuinua mdomo na kusema Chelsea sasa ni bingwa, au kuipa asilimia kubwa ya nafasi. Lakini mwendo wake hadi ilipo sasa inaonyesha inakwenda kwa umakini mkubwa.
Conte ni kocha wa aina yake, kocha ambaye hakupewa nafasi hata ya kuongoza ligi hiyo kwa kuwa vinara kama Jose Mourinho, Pep Guardiola wakiwa wameonja raha ya ubingwa England, Italia, Hispania na Ujerumani, ilionekana isingekuwa rahisi kutamba juu yao.
Leo taratibu anaanza kujipambanua kwamba ndiye kocha mwenye rekodi ya kubeba ubingwa wa Italia miaka mitatu mfululizo akiwa mchezaji katika kikosi cha Juventus. Akarejea na kufanya hivyo miaka mitatu mfululizo akiwa na Juventus hiyohiyo, safari hii akiwa kocha.
Hadi sasa, Conte ana tuzo mbili za Kocha Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu England na mwendo wa Chelsea unaonyesha iko vizuri kuendelea kupambana na iko makini kweli.
Conte ni kocha asiye na jina England, lakini ni yule ambaye mbinu za mpira anazijua hasa tangu akiwa mchezaji wa Juventus ambako alicheza na wachezaji kibao kama Zinedine Zidane, Alessandro Del Pierro, Andrea Pirlo, Edgar Davids na wengine ambao walikuwa mafundi hasa.
Hata kufundisha, kuna wachezaji wengi wakiwemo wale aliowatengeneza na kuwa bora kama Paul Pogba, Alvaro Moratta au aliofanya nao kazi na leo ni magwiji kama Carlos Tevez, Pirlo mwenyewe na wengine wengi.
Conte ni aina ya kocha mwenye uwezo mkubwa wa kuwatengeneza wachezaji na kuamini kila kisichowezekana kinawezekana. Aina yake ni mtu asiyekubali kushindwa na hutulia pale anapoona amefanikiwa kupata ushindi.
Ni kocha mwenye mbinu za uhamasishaji wa juu, na tangu alipokuwa mchezaji, alisifiwa katika upangaji walinzi wakati wakishambuliwa. Wakati fulani alipewa unahodha kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kuwaongoza na kuwapanga wenzake.
Wastani wake wa ushindi tangu ameanza kuwa kocha ni zaidi ya asilimia 55. Wastani wa kupoteza uko chini, ni asilimia 17.2. Hii ni sehemu nyingine ya kuonyesha ubora wake. Utaona Conte anaingia kwenye kundi la makocha bora ingawa alitua England akionekana asingeweza kuwa na nafasi hata kidogo.
Sasa wengi wameshituka wakati tayari amepiga hatua na gari lake limepata moto. Wengi wanajua ubora wake wakati akiwa amekaa vizuri akiwa anaelekea kupambana kupata ubingwa.
Wakati mwingine ni vizuri ukianza kwa kudharaulika, maana unakuwa na nafasi ya kwenda mbali na kufanya vizuri zaidi. Wakishituka unakuwa umeshafika mbali zaidi.
Conte ana ushindani mkubwa kutoka kwa Klopp ambaye ni mmoja wa makocha wapambanaji na ukumbuke alifanya vema akiwa Ujerumani. Alipotua amepata muda wa kuisoma Ligi ya England.
Klopp pia ni bora zaidi kwenye ushambulizi kwa maana ya kasi na upachikaji mabao. Timu yake ndiyo inaongoza kwa kufunga England, katika mechi 17 imefikisha mabao 41.
Maana yake kama ataweza kuimarisha safu yake ya ulinzi, ushindani dhidi ya Conte utaongezeka na kufanya mambo kuwa magumu zaidi.
Makocha wazoefu zaidi kama Mourinho na Guardiola, hauwezi kuwabeza kwa sasa. Mwendo wa Conte lazima unawanyima usingizi na hakuna ubishi, watakuwa wanajuta kumdharau mapema wakimuona wa kawaida kwa kuwa wamempa nafasi ya kuwa pazuri na kuonekana tishio kwao.
Antonio Conte
Umri: Miaka 47
Klabu alizocheza
1985-1991: Lecce
1991-2004: Juventus
Timu ya taifa, Italia
1994-2000: Mechi 20
Timu alizofundisha
2006-2007: Arezzo
2007-2009: Bari
2009-2010: Atalanta
2010-2011: Siena
2011-2014: Juventus
2014-2016: Italia
2016-sasa: Chelsea
Mataji akiwa kocha
Bari: Serie B (2008-09)
Juventus
Serie A: 2011–12, 2012–13, 2013–14
Supercoppa Italiana: 2012, 2013











0 COMMENTS:
Post a Comment