Na Saleh Ally
MIAKA mitatu iliyopita, Simon Happygod Msuva alikuwa kati ya wachezaji wa Yanga waliokuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu, lakini ameonyesha ni mtu anayejua anachokifanya.
Msuva alipata nafasi ya kucheza katika kikosi cha wakubwa Yanga baada ya kuaminiwa na aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana na baadaye timu kubwa, Kim Poulsen, raia wa Denmark.
Poulsen alionyesha imani kubwa kwa Msuva na Frank Domayo ambao ndiyo walikuwa wanachipukia. Hii ikachangia kwa kiasi kikubwa Kocha Ernie Brandts, raia wa Uholanzi, naye kuongeza imani kwa wachezaji hao wawili na kuanza kuwapa nafasi.
Sifa kuu ya mashabiki wa soka nchini, kila mmoja hupenda kuonekana anajua kuliko mwingine na anayelaumu sana ndiye huwa anaonyesha mapenzi kwa klabu yake au mjanja sana.
Msuva kalaumiwa, wakati mwingine hadi anatia huruma lakini ameendelea kuwa mvumilivu. Hakika kuna mambo kwake yalikuwa magumu kufanyika au kutokea kwa kuwa uwezo wake kiuchezaji haukuwa ukimruhusu mambo hayo kutokea au kufanyika.
Alitakiwa kusubiri muda fulani huku akiendelea kujifunza, alitakiwa kuendelea kupambana ili abadilike. Soka si masomo ya darasani, soka asilimia 90 ni vitendo na mtu anatakiwa kujifunza huku akifanya.
Hakuna anayeweza kukataa kwamba kwa misimu mitatu sasa, Msuva amekuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha Yanga ukianza na ule msimu aliokuwa mfungaji bora, wakabeba ubingwa.
Msimu uliopita, kazi yake ilionekana, pia wakabeba ubingwa. Sasa msimu huu, pia anaonyesha ni msaada na anaweza kuendelea kufanya vizuri kwa kuwa tayari ana mabao tisa, yeye na Shiza Kichuya ni vinara wa mabao hadi mechi 16 za Ligi Kuu Bara kwa kila timu.
Achana na masuala ya ushabiki wa Yanga na Simba, tunazungumzia Utanzania. Msuva ni mdogo wetu, ni kijana ambaye akiendelea kufanya vizuri ataitangaza nchi yetu, ataisaidia timu yetu ya taifa, huyu ni mtaji mzuri wa Watanzania hasa kama utatumika vizuri.
Unaweza kutumika vizuri kama mwenyewe atajitambua na kujua kwamba kila kitu kina hatua. Alipofikia leo hii Msuva, anastahili kusonga mbele zaidi kwa kuwa Yanga haiwezi kuwa mafanikio ya mwisho.
Wala siku nyingine kutoka Yanga kwenda Simba, hayawezi kuwa mafanikio ya mwisho. Kama Msuva ametamba kwa misimu mitatu katika kiwango kizuri, kwa nini asiwe na soko au kupata nafasi ya kucheza nje ya nyumbani?
Tukubaliane hivi; kucheza ni jambo moja, nidhamu ni jingine. Suala la masoko ni muhimu zaidi kwa kuwa hata makampuni makubwa ya bidhaa mbalimbali duniani yanajitangaza. Msuva lazima awe na uongozi wake unaofanya kazi ya kuzitangaza kazi zake na kuonyesha ubora wake.
Ubora wake ni mzuri lakini duniani kuna wachezaji wengi sana. Wapo wanaoweza kushindwa kujua anachokifanya Msuva kwa kuwa hana kitengo bora ambacho kingefanya kazi ya kuutangaza zaidi ubora wake.
Kama angekuwa na meneja bora, leo tayari angekuwa amesambaza kazi zake akiwa ametengeneza video bomba kabisa ambayo inaonyesha mabao ya Msuva, pasi, rekodi zake na kadhalika. Hii ingesaidia kwa kiasi kikubwa wengi kumfikia na kutaka kujua kama wanaweza kufanya naye kazi.
Wachezaji wengi wa kiwango chake, wamewahi au wapo wanaofanya kazi hapa nchini na wanalipwa kuliko yeye. Sasa kwa nini naye asiende kwingine akalipwa zaidi na kuleta mabadiliko kwa kupata maendeleo yeye binafsi na kulisaidia taifa letu kama changamoto, au sehemu ya kuwahimiza wengine wanaosaka maendeleo kupitia soka, kwamba inawezekana kwa kuwa yeye atakuwa ameweza?
Kama mtaniita mbaguzi sawa, lakini niwe wazi, ningependa kuona vijana wengi wa Kitanzania wakipiga hatua hasa kwa wale ambao wanakuwa wanaonyesha mfano wa kutaka kufanikiwa. Hii ni mara ya pili naandika kuhusu Msuva na suala la kusonga mbele zaidi, ndiyo maana nataka anikumbushe, kipi anachosubiri?







0 COMMENTS:
Post a Comment