December 9, 2016


Na Saleh Ally
YANAYOTOKEA katika michezo, hakika mengi yamekuwa ni kero kuu na wanaohusika wanakuwa ni wengi wanaoangalia maslahi binafsi kuliko yale ambayo baadaye yanaweza kuwa faida ya watu wengi.

Nimeelezwa kwamba kuna mtu aliwashawashi wachezaji Jonas Mkude na Ibrahim Ajibu kuacha kusaini mkataba mpya na Simba ili waende wakacheze Afrika Kusini baada ya mkataba wao kwisha.

Mtu huyo, sijui ni meneja au wakala amewashawishi wafanye hivyo kwa kuwa tu ana maslahi yake binafsi na anachotaka kitakachopatikana, iwe ni faida yake yeye na wala si Simba.

Mtu hiyo, sijui ni Mtanzania au Mzungu kutoka nje ya Tanzania ambaye anataka kuchuma kutumia wachezaji Waafrika, anachoangalia hapo yeye ni kupata fedha nyingi.
Maana Mkude na Ajibu wakiwa na mkataba na Simba, klabu ndiyo itafaidika katika masuala la malipo. Hivyo huyo wakala anawashawishi Mkude na Ajibu ili faida iwe kwake bila ya yeye kujali namna ambavyo Simba imetoka mbali na hao vijana, imewalea na mwisho kuchangia kuwapandisha thamani hadi unapofikia usajili, leo wanaweza kuomba zaidi ya Sh milioni 50 ili wamwage saini, si kitu kidogo.


Ajabu, Mkude na Ajibu nao wanaona hilo ni sawa, nao wanaingia mkenge bila ya kujiuliza kwa ufasaha kwamba kweli kutokuwa ndani ya timu ndiyo urahisi wa kupata timu?



Hawajiulizi kuwa wachezaji wangapi wametokea Simba, wakapewa ruhusa na leo wanatamba mfano wa Mbwana Samatta. Sasa vipi ukiwa mchezaji huru pekee ndiyo unaweza kupata timu, haupati hofu na uwezo wako.
Achana na hivyo, yaani huyu Mkude na mwenzake Ajibu, hawafikirii kwamba huyo ambaye anawataka kutosaini mkataba ili wawe huru, anataka kujifaidisha zaidi huku Simba ambayo imekuwa nguzo ya wao kufikia walipo haitapata lolote.


Hivi ni kweli, Ajibu na Mkude wanaweza kuiona Simba ni adui au kufanya kila wanaloweza ili isipate kitu. Wakasahau yote waliyopitia wakiwa na klabu hiyo iliyowalea na kuwasainisha mikataba wakiwa makinda kabisa!
Mkude alikiri kwamba aliwazimia Simba simu kwa kuwa mmoja wa viongozi alizungumza na chombo cha habari na kusema walishamsainisha naye akaanza kusumbuliwa na ndugu zake kuhusiana na suala la usajili huo. Hakufafanua ndugu walimsumbuaje. Kuona hivyo, viongozi wa Simba, nao wakaona watafute njia mbadala.


Viongozi Simba wamejua kama haiwezekani tena, basi kuna kila namna ya kuhakikisha wanasonga mbele na lazima wapate mbadala wa Mkude.

Wamemleta kijana James Kotei ambaye amewahi kucheza soka ya kulipwa nchini Oman. Huyu amekuja nchini kwa ajili ya kuisadia Simba katika nafasi ya kiungo mkabaji, yaani namba sita ambayo ilikuwa ‘inamilikiwa’ na Mkude.

Kama unakumbuka, Simba haikuwa na shida ya namba sita. Hata Kocha Joseph Omog alipendekeza Simba kusajili beki wa kati, kipa na mshambuliaji mmoja na wala si kiungo. Kutokana na Mkude kuzima simu, kuwadengulia wameamua kutafuta njia ya kurekebisha kinachowakabili.



Hata kama wako waliomtetea Mkude, au wale wanaomtetea lakini leo kwa mara nyingine mimi nataka kumueleza kwamba uamuzi wake katika suala siriaz, yeye alitanguliza ‘utoto’.

Kama Mkude angekuwa anataka kuondoka Simba, bado alikuwa anaweza kukaa mezani na viongozi na mwisho kukubaliana nao. Mkataba wa muda mfupi unawezekana badala ya kuendelea kupakimbia kwenu, eti kisa watu wanataka kuzungumza na wewe.

Katika sehemu ya kazi, suala la ubora ni muhimu. Lakini uhusiano wenye maelewano ni jambo bora zaidi na linasaidia kuboreka kwa utendaji wa wahusika badala ya kutengenezeana hali ambayo inapunguza uaminifu na upendo.

Simba imekuwa na Mkude muda mwingi zaidi ya wakala wake. Pia Simba inaweza kujua umuhimu na thamani ya MKude kuliko huyo wakala.

Najua kipindi hiki unaweza kuwasikia Mkude au Ajibu wakisema hawakuwahi kufanya kama inavyoelezwa hata kama viongozi wa Simba walilizungumza hilo.

Unaweza kusema mwisho hasa upande wa kiungo wamesababisha Simba kuingia gharama ya kumsajili mtu mwingine ambaye hakuwa kwenye mpango na hata kama watakubali kusajiliwa tena, huenda dau lao likashuka kwa kuwa Simba imelazimika kumwaga fedha ghafla tena katika bajeti isiyotegemewa.

Kuna haja ya wachezaji kujifunza, kwamba hata mawakala nao ni binadamu, wanaweza kukosea. Mawakala pia kila wanachokifanya na mchezaji, mara nyingi huangalia watafaidikaje wao zaidi hata kuliko ya wahusika, yaani wachezaji. Katika biashara ya mchezaji, timu inastahili kufaidika, mchezaji ni namba moja.



3 COMMENTS:

  1. Uko sahihi sana Kaka, Mi binafsi nimekuelewa mno, bila shaka Mkude anapaswa kuona mawazo haya ili yamjenge na afike mbali zaidi kule ambako kila Mchezaji angependa kufika.

    ReplyDelete
  2. Uandishi uchwara usioendana na maadili ya kiuajdishi,mkude kaeleza kwa ufasaha kabisa ishu yake na simba na sote tumemsikia vizuri,haya maneno mnayoleta nyie waandishi msiojua mpira ndio mtaharibu kila kitu,nasisitiza tena mkude tulimsikia kwa mdomo wake akielezea jambo hili.

    ReplyDelete
  3. Bwana Saleh uandishi wako umeegemea upande wa lawama ukakwepa ukweli na haki. Katika soka la kibiashara wachezaji wana thamani zao kulinganisha na huduma au viwango vyao. Mkude anaona thamani yake ni milioni 80 Simba wanaona kiwango chake ni milioni 50! Naomba kulezwa Kotei kalipwa milioni ngapi? Zisingetosha hizi kumuongezea Mkude ili kumuongezea morali na kumtunuku kwa uzalendo na huduma nzuri ya muda mrefu? Naamini Kotei kaletwa kama kumkomoa Mkude ile keamba mke jeuri muolee mwenzie! Simba wanataka kuusahau mbachao kwa msala wa muda tu tena wa kighana! Hizo pesa alizolipwa Kotei zitakwenda Ghana kama dola si bora zingewafaa waluguru wetu au ndo ile kwamba bora kioze kuliko kumpa jirani?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic