Na Saleh Ally
JANA Tanganyika ilikuwa imetimiza miaka 55 ya uhuru na sherehe ya maadhimisho ilifanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.
Miaka 55 ni mingi na wakati mwingine ni vizuri zaidi kupima wingi wa miaka na mafanikio yako. Tunaweza tukajiuliza mengi sana kuhusiana na michezo na soka, ndiyo unadidimia kwa kasi ya kimondo.
Wakati Tanganyika inatimiza miaka 55, hakuna ubishi tena kwamba michezo upande wa Tanzania Bara ni hovyohovyo, tena kupita kawaida.
Mchezo wa soka ambao ni maarufu, uko ICU (chumba cha wagonjwa mahututi), katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Tanzania iko katika nafasi ya 160.
Wakati tunazidi kuchanganyikiwa na kuporomoka, habari mbaya zaidi ni kwamba Jamal Malinzi ana mpango wa kutetea nafasi yake hiyo kwa mara nyingine, jambo ambalo unajiuliza, sasa ni hivi, akiongoza tena kwa miaka zaidi ya mitatu, soka litakuwa wapi? Maana yake ni mwisho wa safari, yaani si ICU tena, kaburini kabisa.
Maajabu ya mambo ambayo hayahusiani na mchezo wa soka yanazidi kupamba moto huku yakiashiria kwamba hakuna nafasi ya maendeleo ya mchezo huo, tena na wadau rundo, wamekaa kimya kama wameususa.
Tanzania inalia na waamuzi kwamba wana kiwango cha chini kabisa, maana yake zinatakiwa kufanyika juhudi za makusudi kukuza viwango vyao.
Wakati bado kuna changamoto kubwa kwa waamuzi kwamba wana viwango duni kabisa, kuna watu wanaojiita ni wadau wa soka nchini, eti ambao hawajataka kutajwa majina yao, wameamua kumpa zawadi ya gari mwamuzi Jonesia Rukyaa kwa kuwa alichezesha vizuri michuano ya Kombe la Mataifa la Wanawake kati ya Ghana na Afrika Kusini, ilikuwa mechi ya mshindi wa tatu.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF, ni kwamba mwamuzi huyo kutoka mkoani Kagera, alichezesha mechi hiyo na kuonekana hana upungufu katika suala la Sheria 17 za Soka, hivyo wadau hao wakatoa zawadi ya gari aina ya Toyota Vitz.
Wakati tukiwa katika mjadala wa kawaida kuhusiana na zawadi hiyo, mmoja wa marafiki zangu aliniuliza maswali kadhaa ambayo yote sikukubaliana naye kwa kuwa sikuwa nimelenga hayo.
Alishangazwa kuona mwamuzi anachezesha mechi moja ya kimataifa, basi anatuzwa gari. Akauliza je, ni kwa kuwa anatokea Kagera ambao ni mkoa anaotokea Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera (KRFA), Jamal Malinzi ambaye pia ni Rais wa TFF, pia ndiyo mkoa anaotokea Katibu Mkuu wa shirikisho hilo! Na ndiyo mkoa anaotokea mshauri wa masuala ya ufundi wa rais wa shirikisho hilo pia.
Nikamueleza kuachana na hisia hizo ambazo niliona mtu anaweza kudhani ni ubaguzi, lakini kila mtu ana haki ya kuhoji. Nikaheshimu mawazo yake, lakini nikaacha yawe maswali maana sikuwa na majibu!
Akaniuliza tena, vipi wadau wanajificha, wanahofia nini? Vipi wadau wanatoa zawadi kwa mwamuzi aliyefanya vizuri mara moja tu, kwani hakuna mwamuzi aliyechezesha michuano ya kimataifa akafanya vizuri? Au kwa kuwa ni mwanamke, wamemuonea huruma? Ni ndugu zake, wanatokea mkoa mmoja? Nikamueleza sina jibu na sijalenga huko.
Nilikolenga mimi ni kuonyesha kiasi gani mpira umejaa propaganda na salamu zangu hizi ziwafikie wadau kokote walipo, kokote walipojificha kwa kuwa najua zitapenya tu kwamba sisi ni watu wenye akili zetu timamu na wasitufanye majuha.
Zawadi ya gari kwa mwamuzi aliyechezesha mechi moja ya kimataifa? Huku tasnia ya waamuzi ikiwa imeyumba na kunatakiwa juhudi za makusudi kuwainua wengine kwa maana ya mafunzo ya mara kwa mara au ikiwezekana hata kuwaalika wakufunzi wa kimataifa kuja nchini kuwapiga msasa mara kwa mara ili kuboresha kiwango chao.
Waamuzi wanakosea mara nyingi, lakini tunajua wanavyokuwa na wakati mgumu pale wanapolazimika kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Wanakuwa hawajui kipi ni sahihi cha kufanya.
Kumtuza mwamuzi gari huku tukijua wako wengi wamechezesha nje ya Tanzania na hakukuwa na malalamiko, hawakupongezwa hata kwa maneno tu! Hii si sawa hata kidogo.
Sitaki kuingia kwenye hisia za rafiki yangu, kwamba hawatokei Kagera! Lakini tukubali kuna upungufu wa wazi ambao hauleti picha nzuri na ndani ya TFF mambo yamekuwa yakiendelea kwa mfumo huo bila ya hofu, aibu wala kujali.
Awali, niliwahi kusema, Malinzi alipaswa kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti KRFA, maana hata wakati anamkabidhi gari mwamuzi huyo, unakuwa haujui anamkabidhi akiwa mwenyekiti wa chama cha mkoa au rais wa shirikisho? Pia hiyo hali ndiyo inayozaa zile hisia za conflict of interest (mgongano wa maslahi).
Inawezekana nia ya Malinzi ni nzuri kabisa, lakini yeye kutokea Kagera pia inaweza kuzua shida kwa kuwa ni mwenyekiti pale. Hivyo lile suala la kuachia KRFA, leo ninalikumbusha tena. Kwamba hata kama katiba inaruhusu, kwa kuwa muungwana ni vitendo au ile methali ya “Inafaa kusema mgomba ungali wima”. Yaani vizuri kusema wakati jambo likiwa moto, usisubiri.
Hata kama wadau nao hawataki kutajwa, basi vizuri kujipima, pia mjue Watanzania wameamka na wanajua mengi yakiwemo yale ya nyuma ya pazia. Kupeana tuzo ni jambo jema, lakini hata wadau wasiotaka kutajwa, nao wajifunze kwamba zawadi nyingine hasa zisipopita kwenye njia sahihi, huvunja watu wengine mioyo na kuwamaliza kabisa.
Rahisi sana kusema wadau wasiotaka kutajwa, lakini dunia hii haina siri tena. Ni rahisi kujua wadau hao ni kina nani na wanatokea wapi halafu baada ya hapo, watu wataumia, watavunjika mioyo na kuzidi kuufanya uwezo wa waamuzi kuzidi kudidimia.
Kutoa zawadi ni jambo zuri, lakini tukubali wakati mwingine kuna sababu za kupima, unatoa wapi, nini na wakati gani na kwa faida ya nani na tujue viongozi wapo kuendeleza michezo nchini na si sehemu fulani tu.
Miaka 55 ni mingi sasa, inawezekana walioanza walikuwa na upungufu. Basi waliopo sasa nao warekebishe badala ya kuzidi kuharibu hata kuliko waliopita.
0 COMMENTS:
Post a Comment