January 7, 2017Kuhusu ile kasi ya Simon Msuva wa Yanga kuzifumania nyavu kwa sasa, imemfanya straika Amissi Tambwe kusema ni kosa kumfananisha winga huyo na kiungo mshambuliaji yeyote nchini hata Shiza Kichuya wa Simba.

Msuva hadi leo ana mabao manne katika Kombe la Mapinduzi baada ya kucheza mechi mbili, wakati katika Ligi Kuu Bara ana mabao tisa akiongoza kwa ufungaji na Kichuya na Tambwe wenye idadi kama hiyo ya mabao.

Tambwe amesema kuwa, Msuva kwa sasa anatisha na yupo vizuri kuliko mawinga wote hapa nchini akiwemo Kichuya kwani kiwango chake kipo juu na anaweza kuwa mfungaji bora wa ligi kuu na Kombe la Mapinduzi.

“Nampongeza sana Msuva kwa kazi yake nzuri ambayo anaifanya uwanjani tangu tumefika Zanzibar  na kufanikiwa kuongoza katika msimamo wa wafungaji.

“Najisikia raha sana juu ya hilo na nina tamani kasi yake hiyo isipungue mpaka mwisho wa michuano ili aweze kuibuka mfungaji bora kwani hakuna winga yeyote nchini ambaye unaweza kumlinganisha naye, hata Kichuya hamkuti,” alisema Tambwe.


Endapo Msuva atafanikiwa kuibuka mfungaji bora wa Kombe la Mapinduzi mwaka huu, hiyo itakuwa ni mara yake ya pili ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2015.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV