January 19, 2017

Wakati mashabiki wengi wa Simba wanaonekana kuingiwa hofu, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amewataka kuendelea kuungana kwa kuwa watani wao Yanga watakuwa wanacheza kwenye ile hadithi ya fisi na mkono.

Hadithi hiyo ni ile mwanadamu anatembea huku fisi akimfuatilia nyuma kwa matumaini mkono wake utadondoka kutokana na anavyourusha kila anapopiga hatua.

“Si unajua ile hadithi ya fisi na binadamu. Maana fisi anamfuata tu binadamu akiamini ule mkono unaweza kuanguka.

“Sasa ndiyo Yanga, watakuwa wanaona pointi zinapungua, mara zinaongezeka, mara zinapungua mara zinapungua hadi mwisho,” alisema Hans Poppe.

“Sisi tunaendelea kupambana na tunawahimiza vijana kuendelea kujituma, mashabiki kudumisha umoja na sisi tunajitahidi kadiri ya uwezo wetu.”

Simba iko kileleni mwa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 45, Yanga inafuatia ikiwa na 43.

Baada ya sare dhidi ya Mtibwa Sugar, Yanga ikawa inazidiwa na pointi mbili tu.


Hali hiyo inaonyesha imeamsha hamasa kwa mashabiki wa Yanga wakiamini kwa kuwa Simba inakwenda kucheza na Azam FC, basi wao ni nafasi za kuivuka Simba.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV