Katika Kikao cha Bodi ya Kusimamia na Kuendesha Ligi, kiliketi mwanzoni mwa wiki hii na kufanya tathmini ya mambo mbalimbali yaliyotokea kwenye michezo mbalimbali ya mpira wa miguu kwa michuano yote – Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.
Baada ya kikao hicho, kumetolewa adhabu kadhaa na baadhi ni hizi zifuatazo.
Klabu ya Bulyanhulu FC imepigwa faini ya Sh 300,000 (laki tatu) baada ya timu yake kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.
Waamuzi wa mechi hiyo; Mwamuzi Elikana E. Mhoja (Mwanza), Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, John Mrisho (Mwanza), na Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili, Mukhusin I. Abdallah wa Mwanza wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa kushindwa kumudu mchezo huo. Uamuzi dhidi yao umezingatia Kanuni ya 38(1a) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
Pia timu ya Bulyanhulu FC ilichelewa kufika kwenye kikao hicho katika mechi namba 28 dhidi ya Milambo FC iliyofanyika kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.
Mechi namba 30 (Mawenzi Market vs Sabasaba United). Klabu ya Mawenzi Market imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na maofisa wawili tu badala ya wanne, na pia kutokuwa na vifaa vya mchezo. Adhabu dhidi ya klabu ya Mawenzi Market imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.
Mchezaji Awadh Ahmed wa Sabasaba United amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kumsukuma Mwamuzi na kugoma kutoka uwanjani baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 37(7) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
0 COMMENTS:
Post a Comment