Nahodha na beki wa kati wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro', ametamka kuwa kati ya makosa ambayo hawataweza kuyafanya basi ni kutoka kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara huku akiwaambia Simba kuwa wasubirie hadi msimu ujao.
Beki huyo mkongwe aliitoa kauli hiyo baada ya timu yao kuitoa Simba kileleni kwenye msimamo wa ligi kuu. Simba iliongoza msimamo huo kwa muda mrefu lakini ghafla imeshtukia ikishushwa.
Yanga hivi sasa inaongoza kwenye msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 49 huku Simba wakiwa nafasi ya pili na pointi zao 48 baada ya kushinda juzi Jumamosi mechi na Majimaji.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Cannavaro alisema anafurahia malengo waliyoyaweka ya kuhakikisha wanawatoa kileleni Simba kabla ya kukutana nao Februari 25, mwaka huu, yametimia.
Cannavaro alisema walichopanga ni kuendelea na kasi waliyonayo ya kufunga kila mechi watakayoicheza ili waendelee kukaa kileleni hadi mwisho wa ligi.
Aliongeza kuwa, hilo linawezekana kwao kutokana na ubora wa kikosi chao na maandalizi ya kila mchezo wanayoyafanya chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina.
“Moja ya mipango tuliyokuwa nayo kuanzia wachezaji na benchi la ufundi, ni kupambana kuhakikisha tunaendelea kubaki kileleni kwenye msimamo wa ligi kuu.
“Hiyo ni baada ya kuwaondoa kileleni Simba katika nafasi hiyo waliyokuwa wanaiongoza tangu mwanzoni mwa ligi kuu, hivyo baada ya kufanikiwa kukaa juu, basi hatutakubali kutoka kileleni hadi mwishoni mwa ligi.
“Ninafurahi mwenendo mzuri wa timu yetu ambayo kila siku inaonyesha kubadilika kwa kucheza soka safi na lenye ushindani," alisema Cannavaro.
0 COMMENTS:
Post a Comment