Na Saleh Ally
MECHI ya leo ya watani, Simba dhidi ya Yanga inasubiriwa kwa hamu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo itakuwa na mambo mengi yakiwemo yale ya kushitua kwa kuwa hakuna aliyetarajia, lakini kuna makosa mengi ambayo hufanyika.
Kati ya makosa hayo, 10 yafuatayo yanaweza kutokea na ikiwa hivyo, basi kuna upande utamwaga machozi kwa kuwa mechi yenyewe ilivyo, inaonekana kama hakuna sare, kuna upande utaumia.
Mavugo, Bossou:
Kuna tatizo litatokea hasa kama Laudit Mavugo atakuwa katika kiwango kizuri. Kama Kelvin Yondani atasogea mbele yake kumuacha abaki na Vincent Bossou, haitakuwa rahisi kwake.
Achana na zile mbwembwe za Hamisi Kiiza dhidi ya Bossou. Mavugo ni tofauti ingawa Bossou anaweza ‘kumuwini’ kwa kumgonga kila mara na hiyo itakuwa hatari kwake kwa kuwa Mathew Akrama ni mwamuzi mkali na mwepesi wa kutoa kadi.
Kasi ya Mavugo, si rahisi Bossou kuihilimi, pia ni mchezaji mtundu na mjanja anapoingia kwenye boksi. Yondani, akianza naye itakuwa vema zaidi na Bossou amalize, vinginevyo ni kosa.
Juma Abdul, Liuzio:
Yanga inamtegemea Juma Abdul kupanda na kupiga krosi murua zenye ‘macho’. Kama Kocha Joseph Omog ataamua kuanza na Juma Liuzio namba 11, basi ni hatari kubwa kwa Yanga kumruhusu Abdul apande.
Kama akifanya hivyo, lazima iwe kwa machale sana kwa kuwa Liuzio amekuwa fiti na mwenye kasi zaidi.
Kitu kingine, inaonekana Abdul kama ameongezeka kilo. Hivyo hawezi kuwa na ile kasi ya mwanzo. Kuliko kwenda kupiga krosi mara nyingi zaidi, basi anaweza kubaki na kulinda zaidi.
Pasi za Kotei, Zulu:
James Kotei wa Simba ni mmoja wa wachezaji wanaopiga pasi nyingi zinazofika. Ndiye mchezaji anaongoza kwa kupiga pasi nyingi ndefu zinazofika.
Hali kadhalika kwa Yanga, Justine Zullu, amekuwa akipiga pasi nyingi ndefu kwa Simon Msuva au Obrey Chirwa na zimekuwa zikifika pia.
Kwa walinzi wa kati wa Yanga au Simba, lazima wawe makini na uanzishwaji wa pasi kutoka kwa viungo hao.
Mara nyingi wanaopewa pasi hizo wanakuwa na kasi hivyo kufanya shambulizi kuwa la kushitukiza. Wasio na kasi kama Bossou au Novaty Lufunga wakiwa uwanjani, wanapaswa kuwa makini zaidi.
Zimbwe Jr, Msuva:
Msuva na Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’ wanajuana. Kitu kizuri zaidi wote wako katika viwango vizuri zaidi tangu kuanza kwa mzunguko wa kwanza.
Kitakachotokea hapa ni kuviziana. Atakayefanya kosa basi ameumia. Kosa linaweza kuanzia kwa Msuva kutoshuka kumsaidia Abdul au litaanzia kwa Zimbwe Jr akienda kushambulia akamsahau Msuva nyuma.
Niyonzima iwe Kaseke:
Kocha wa Yanga, George Lwandamina anaweza kuanza na Deus Kaseke au Juma Abdul ili kufanya mashambulizi ya mfululizo. Ikifanikiwa inaweza kuwa vizuri lakini litakuwa kosa kubwa ikikataa kwa kuwa Haruna Niyonzima yuko katika kiwango kizuri zaidi.
Baadaye angeweza kuutuliza mpira lakini ‘chemistry’ yake sasa na wachezaji wengine imekaa vizuri zaidi na vema akaanza.
Kichwa cha Tambwe:
Kwa misimu mitatu sasa hakuna mchezaji anapiga vichwa hatari kama Amissi Tambwe. Kama mabeki wa Simba watampa nafasi hata tatu, ana uwezo wa kuwaadhibu mara mbili. Ni lazima kuhakikisha hapigi kichwa hata kimoja.
Kwani hata katika wakati mgumu wa ulinzi, Tambwe ameweza kufunga mabao ya kichwa. Kumzuia inatakiwa zaidi ya akili.
Krosi za Bokungu, Juma:
Hadi sasa, Abdul na Janvier Bokungu ndiyo mabeki wanaopiga krosi hatari kabisa kwenye malango ya upinzani.
Kasi kubwa kwa Liuzio na Niyonzima au Kaseke, atakayeanza ni lazima afanye kazi kuhakikisha hawapati nafasi ya kupiga krosi nyingi. Kuwaacha wafanye kazi hiyo, itakuwa kosa kubwa kwa kila upande.
Usisahau, Haji Mwinyi kwa Yanga na Zimbwe Jr kwa Simba, wameimarika sana. Wamekuwa wakipiga krosi zilizozaa mabao, maana yake hatari ya krosi iko juu zaidi.
Mashuti ya Ndemla, Mahadhi:
Wako wachezaji wanaoweza kupiga mashuti ikawa hatari. Mfano Niyonzima au Mavugo, si wa kuwaachia.
Chipukizi hawa Said Ndemla au Juma Mahadhi ni hatari zaidi. Wakipata nafasi wanaweza wakasababisha madhara upande wa upinzani.
Wana sifa ya kutafuta nafasi ya kupiga kwa kuipasua safu ya ulinzi. Hivyo ni lazima kuhakikisha “the block”, kinakuwa mbele yao. Wakiachiwa, ni kosa kubwa.
Kulalia kwa mwamuzi;
Mechi nyingi za Yanga na Simba, huwa zinaharibiwa na jazba. Kama katika mechi ya leo, wachezaji watapeleka akili zao kwa mwamuzi, basi watajitoa mchezoni.
Akrama ni mkali na asiyesita kutoa kadi. Kama binadamu anaweza kukosea na wachezaji wanapaswa kulikubali hilo. Waking’ang’ania mwamuzi, basi watajitoa mchezoni.
Kumbuka mechi ya mzunguko wa kwanza, baada ya Tambwe kufunga kabla akiwa ameshika. Kwa takribani dakika 10, Simba hawakuwa mchezoni. Mwisho bado dakika 8, ndiyo walionekana kurejea na kushambulia mfululizo.
Hofu:
Hofu imekuwa adui wa burudani katika mechi hii, wachezaji wachache sana kama Niyonzima wanaweza kuonyesha utulivu na kucheza wanavyotaka kwa usahihi.
Kwa hofu, ubunifu wa wachezaji hupungua, kila mmoja anakuwa na hofu, hataki kubaki na mpira hata sekunde.
Lazima wachezaji wakiamini na kucheza soka sahihi, waonyeshe ukomavu na kuutumia ubunifu walionao kuzisaidia timu zao.
Makocha nao huwa waoga katika mechi kama hizi. Hofu yao inafanya wabadili mifumo na huenda wakaanza kwa kujilinda sana na hasa Omog. Hili nalo huwa kosa kwa kuwa kama wanaolinda wakifungwa, kufunga kwao inachukua muda.
Vizuri makocha wakapunguza woga na kuachia timu zicheze tahadhari hasa zinapopoteza mpira.
0 COMMENTS:
Post a Comment