February 26, 2017



Na Saleh Ally
Yanga ya sasa inaweza kuwa na uongozi imara ulioifanya isonge mbele na mambo yake mengi kwenda vizuri.

Utaona ndani ya Yanga umoja umekuwa juu zaidi na imefanikiwa katika mambo mengi.

Lakini inaonekana, Yanga hii si ile ya zamani na inaweza kuchezewa hovyo na yoyote.

Wachezaji kadhaa wa kigeni wameonekana kuichezea Yanga nayo imekuwa ikikaa kimya bila ya kusema lolote ikionyesha kuwa na hofu.

Achana na kwamba Yanga imeshindwa kutamba mbele ya Simba ambayo ilishinda kwa mabao 2-1 dhidi yake.

Lakini unaona, wachezaji kadhaa wa kigeni akiwemo Vicente Bossou wameonyesha wazi hawana mpango, wameamua kujiweka kando.

Mshambuliaji Donald Ngoma ambaye ametokea kwao Zimbabwe kuja kufanya kazi Yanga, amekuwa akiwapa wakati mgumu kususa mambo kadhaa.

Kuna taarifa ni majeruhi lakini kuna taarifa kwamba amekuwa akijumuisha hali ya kutofurahishwa na mambo kwa kubaki nje akisisitiza yeye ni majeruhi.

Hakuna kinachoweza kuthibitishwa kwamba kweli ugonjwa wa Ngoma unakuweka nje kwa zaidi ya mwezi.

Lakini zipo taarifa kuwa ana malalamiko, hajafurahishwa na hili na lile au alicheleweshewa malipo yake.

Pamoja na yeye kuwa na malalamiko, wako wengine wenye malalamiko lakini wameendelea kucheza na kuitumikia Yanga.

Wako wachezaji wazawa wenye malalamiko, wako wageni pia wenye malalamiko. Lakini hawa wote wamekuwa wakicheza tena kwa juhudi kuu.

Kumekuwa na shida kwa baadhi ya wachezaji kuonyesha wao ni kama wakubwa dhidi ya klabu na hili linaonekana kuchukua nafasi kubwa ndani ya klabu hiyo.

Ukweli si sahihi, Ngoma, Bossou au mchezaji mwingine hawezi kuwa mkubwa kuzidi Yanga. Ikiwa hilo linaonekana ni sawa, basi hiki ni kichekesho.

Viongozi waache mapenzi na ikiwezekana kuwafanyia kazi ikiwezekana kuwashughulikia wote wanaoleta figisu kwa kuwa wanawaangusha au kuwakatisha tamaa wenzao.

Wanaozingua sasa, baadaye watalipwa mishahara na inawezekana mishahara yao ikawa mikubwa kuliko ya wengine wakiwemo wazawa ambao wanafanya kazi zao kwa juhudi.

Viongozi wawe imara, waache uoga eti ukimgusa Ngoma basi kina fulani au mashabiki watakasirika. Ngoma ni nani? amejiunga na Yanga lini? Kipi kikubwa cha kukumbukwa zaidi ya wengine amekifanya peke yake? Kama ni muhimu vipi hawi msaada kipindi cha matatizo?

Tuache kuhofia watu, tuache kuwatukuza watu ambao wanataka kutukuzwa bila sababu za msingi. Tuzidhamini klabu zetu na ikiwezekana kuwaonyesha wageni sisi ni imara na tunajitambua, anayezingua apewe virago vyake "atambae".

2 COMMENTS:

  1. Relax baba..mbona umepanic na matokeo, unaongea kwa ujasiri et apewe vilago...wenzio wanamjua thamani yake wew unalijua jina lake

    ReplyDelete
  2. kwani anachodai si haki yake tatizo mmezoea vilabu kuendeshwa kiswahili ndio maana unaona mchezaji kunyimwa haki zake ni jambo la kawaida badala ya kulaumu wachezaji waulize viongozi kwanini hawawatimizii wachezaji madai yao

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic