March 13, 2017
Baba mzazi wa mshambuliaji wa kimataifa, Mtanzania, Mbwana Samatta ‘Samagoal’, mzee Ally Pazi Samatta, amefunguka kuwa malengo makubwa kwa mtoto wake kwa sasa ni kuona anafanikiwa kucheza Ligi Kuu England kama anavyotaka mwenyewe.

Mzee Samatta amesema hayo kufuatia mshambuliaji huyo kuendelea kung’ara katika soka la Ulaya baada ya kuweka rekodi kadhaa za kipekee katika michuano ya Europa League kwa kuiongoza timu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji, kuifunga KAA Gent mabao 5-2 katika michuano hiyo, wiki iliyopita huku yeye akifunga mabao mawili kati ya hayo.

Mzee Samatta alisema kuwa anachokifanya kwa sasa mtoto wake ni kuendeleza moto aliokuwa nao wakati anacheza TP Mazembe ya DR Congo kwani ana malengo ya kucheza Ligi Kuu ya England.

“Kiukweli kwangu si kitu cha ajabu sana kwa sababu naona anaendeleza ule moto wake aliokuwa nao  wakati yupo TP Mazembe, jambo zuri kwake ni rekodi kubwa ambayo ameweza kuiweka kwenye michuano hiyo maana wale waliocheza nao wamekuwa wakiwasumbua katika ligi yao.

“Bado sijaongea naye lakini mwenyewe anataka kwenda kucheza Ligi ya England ambapo hiyo ndiyo ndoto yake ya muda mrefu, sasa kufanya kwake vizuri kwenye michuano hiyo, inaweza ikawa njia rahisi ya yeye kuweza kufanikiwa kucheza huko, namuombea hilo lifanikiwe kama ilivyokuwa kwa Watanzania wengine,” alisema Mzee Samatta.

SOURCE: CHAMPIONI.

Seebait.com 2017

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV