March 11, 2017Na Saleh Ally
KWA sasa inakuwa ni vigumu tena kukataa kwamba soka la Ulaya linatawaliwa na Wahispania na Wajerumani.

Hii unazungumzia ngazi ya kimataifa hasa kwa klabu ambazo ndiyo matajiri zaidi katika Bara la Ulaya.

Ligi Kuu England maarufu kama Premier League ndiyo maarufu zaidi kuliko zile za Hispania (La Liga), Ujerumani (Bundesliga) au Italia (Serie A).

Unapoingia kwenye soka la Ulaya. Unaona hakuna timu za England zenye nguvu hasa baada ya kuyumba kwa Man United kulikotokana na kuondoka kwa kocha mkongwe, Sir Alex Ferguson.


Kwa sasa utawala ni Wahispania na Wajerumani. Mfano mzuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, hadi sasa, katika timu nne zilizoingia robo fainali, mbili Bayern Munich na Borussia Dortmund zinatokea Ujerumani na mbili Barcelona na Real Madrid ni za Hispania.

Zinatakiwa nyingine nne ambazo zitazishinda nyingine nne. Katika hizo Hispania ina timu mbili, Sevilla inayocheza na Leicester City ya England na Atletico Madrid inayoivaa Bayer Leverkusen ya Ujerumani.


Hivyo, Ujerumani wanaweza kuingiza timu moja na Hispania moja tena au mmoja akaingiza timu mbili, yote inawezekana.Misimu 18 iliyopita inaonyesha timu za England ni tatu tu zilizobeba ubingwa. Liverpool, Chelsea na Man United chini ya Ferguson mara mbili. Hispania wamebeba mara 10 na Ujerumani mara nne.


Waitaliano mara nane pia, lakini wanaonekana kupotea katika msimu yote nane ya hivi karibuni na Hispania ikitawala kwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa kupitia Madrid na Barcelona, mara tatu mfululizo.

Unaweza kujiuliza ubora wa England na ligi yao uko wapi kama miaka mfululizo timu zao haziwezi kufanya vizuri kwenye ubora wa juu zaidi.


Kwamba zinapokutana na timu za Hispania au Ujerumani au hata Italia, zinaonekana nyanya.

Unakumbuka Barcelona ya Pep Guardiola ilivyoitesa Man United ya Ferguson licha ya kwamba alikuwa kocha mbishi na mpambanaji kwelikweli.


Uchambuzi wa mambo unaonyesha vipaji vya upande wa nchi za Ulaya Kusini ukanda wa Mediterranian viko juu zaidi na nchi za Ureno na Hispania, watu wake wengi kiasili wanatokea Amerika Kusini.

Kwa nchi za Ulaya, Ubelgiji na Uholanzi zinazalisha vipaji vingi zaidi lakini si maarufu kwa mafanikio makubwa kwa ngazi za klabu hata timu za taifa.


England inaonekana kufanikiwa kutengeneza ligi maarufu, tajiri na klabu maarufu kwa maana ya uchumi lakini nguvu ya kipaji, inazidi uwezo wa fedha.

Wajerumani wanaaminika ndiyo Wazungu makini zaidi. Kwao kuna vipaji lakini mambo yao huenda kwa mpangilio zaidi, walio na moyo wa ushindani na ushindi.England tofauti na Hispania hata ukizungumzia aina ya uchezaji lakini wapambanaji na inaonekana wameshindwa kuvunja nguvu ya utawala wa Hispania, Wajerumani au Waitaliano ambao waliporomoka baada ya kutamba muda mwingi.

Man United inaendelea kubaki ndiyo nguzo pekee ya England kwa kuwa ndiyo yenye mafanikio zaidi kwa siku za hivi karibuni na kuyumba kwake, inaonekana kumeiyumbisha England.


Chelsea si maarufu sana, haina mashabiki wengi sana lakini inaonekana kujitutumua. Wakongwe wengine kama Arsenal na Liverpool, wanaongoza kwa kusuasua na afadhali nyingi.


Kwa mwendo ulivyo, ukiangalia msimu huu. Inaonekana utawala wa Hispania, Ujerumani na huenda kufuatiwa na Italia utaendelea kuisumbua England.

Tangu Man United imeyumba, angalau Chelsea ilijaribu na kufanikiwa kubeba ubingwa msimu wa 2011-12 kwa kuitwanga Bayern Munich na Didier Drogba akawa shujaa.Baada ya hapo unaona timu za England zinazoingia kwenye Ligi ya Mabingwa, hakuna inayozisumbua au kuzipa hofu timu za Hispania au Ujerumani na sasa zinagawana tu ubingwa zinavyotaka.England itaendelea kubaki na utawala wa ligi maarufu na tajiri. Ikitaka kutamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, basi ni lazima kuwasubiri Chelsea na Man United warudi, waliopo sasa, ni hadithi tu. 

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV