March 11, 2017

Na Saleh Ally
NILIKUWA nimekaa nyumbani juzi usiku, lengo ni kuangalia mechi za Europa Cup hatua ya 16 timu zikiwa zinawania kucheza robo fainali.


Mechi mbili zilinivuta zaidi, Man United dhidi ya Rostov na ile ya Genk dhidi ya Gent ikiwa nyumbani.

Hizi Gent na Genk zote zinatokea Ubelgiji, ilikuwa kama bahati mbaya au nzuri zikapangwa pamoja.


Man United ni timu kubwa, lazima uifuatilie lakini mwisho niliamua kuachana na mechi hiyo licha ya kwamba ilikuwa muda tofauti na Genk dhidi ya Gent.

Nikasema nitaangalia mechi ya timu hizo kwa ajili ya kumuona Mtanzania Mbwana Samatta akipambana na kwa kuwa ndiye alikuwa amepewa jukumu la kuongoza mashambulizi katika mechi hiyo ngumu ya ugenini, nikasema acha nione hiyo huku nikiwa nimetoa macho na kukapua kwa shida.


Nilifanikiwa kuangalia mechi dakika ya kwanza hadi 90 na Samatta kama kawaida yake, akafanya yake na kufunga mabao mawili wakati Genk iliyo ugenini ikiitungua Gent kwa mabao 5-2 katika mechi hiyo ya kwanza.

Halikuwa jambo jipya kuangalia mechi ya Europa lakini kumuona Samatta akicheza mechi yake ya kwanza ya Europa League katika hatua hiyo ya 16 Bora na kuwa Mtanzania wa kwanza kufanya hivyo.


Kama haitoshi, akiandika rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga mabao katika hatua hiyo.

Niliona mabeki wa Gent walivyokuwa wakisumbuka naye, lakini niliona namna ambavyo uchezaji wake ule akiwa Simba, au hata ule wa TP Mazembe na sasa, ni vitu tofauti kabisa. Hakimbii tena kwa kasi na mpira, hang’ang’anii tena mpira. Badala yake anakaa kwenye nafasi anatoa pasi au kuweka nyavuni.


Kwangu lilikuwa jambo la kujivunia sana, nilisikia raha sana na kuona kumbe inawezekana Watanzania wengine wakafikia hatua hiyo kwa kukubali kuwa Samatta amefanya juhudi kuu, anapaswa kuungwa mkono, kuombewa zaidi na kuigwa.


Tujivunie yeye, walio chini watamani alipofikia kwa kuwa kukaa ukiangalia runinga mubashara, tena Europa League halafu Mtanzania ndiye anakuwa gumzo na tishio huku akiwamaliza watu, si kitu kidogo waungwana.


Kwangu hiyo imekuwa mechi ya kwanza kubwa au ya ‘level’ ya juu kumuona Mtanzania akicheza huku akiwa ndiye kiongozi, staa au tegemeo.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV