March 13, 2017Kikosi cha Simba leo Jumatatu kinatarajia kuingia mkoani Arusha kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa kuwakabili wenyeji wao Madini katika mchezo wa Kombe la FA, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog raia wa Cameroon akitamba kwamba hawatawadharau wapinzani wao hao.

Simba ambao wanapambana kutwaa mataji mawili makubwa msimu huu, watakuwa ugenini katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Madini, mechi ambayo imepangwa kupigwa wikiendi hii mkoani humo.

Omog amesema wameamua kwenda mapema mkoani humo kwa ajili ya kambi ya mapema kujiandaa na mechi hiyo pamoja na kuzoea mazingira kwani ndiyo mara ya kwanza kwenda mkoani humo.

“Hatukuwa na sehemu ya kwenda baada ya kutoka Dodoma tukaona kwamba twende Arusha moja kwa moja kuweka kambi na kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Madini kwa sababu tunataka kushinda mechi hiyo na kutinga hatua za mbele zaidi.

“Kingine ni kwamba hatuwadharau wapinzani kama wengi wanavyoona eti mechi rahisi kwa sababu wao wapo daraja la pili, kikubwa sisi tutawaheshimu na kuuchukulia mchezo huu kwa uzito kama mechi nyingine kwa sababu wamefika hapa kwa uwezo waliouonyesha.

“Ila niwaambie kwamba sisi tunataka matokeo kwa ajili ya kusonga mbele kwenye hatua nyingine na lazima tushinde na hapo ndipo watashindwa kutuzuia kwani ni lazima tushinde hata iweje ili kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Omog.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV