March 6, 2017
Na Saleh Ally
SHABIKI wa Yanga ambaye anaweza kuwa maarufu zaidi kwa kipindi hiki basi ni yule Kanjunju John ambaye alimwaga machozi baada ya kikosi cha Yanga kuchapwa mabao 2-1 na watani wao, Simba.

Kikubwa kilichokuwa kinamliza Kanjunju ni kupoteza fedha zake Sh 50,000 ambazo ‘alibeti’ akiwa na imani kubwa kuwa timu anayoishabikia ya Yanga inaitandika bila hofu hata kidogo.

Wakati mechi inaanza, mambo yalionekana kwenda poa sana kwa Kanjunju, maana Yanga iliongoza kwa bao la penalti la dakika ya tano tu mfungaji akiwa ni Simon Happygod Msuva.

Lakini dakika ya 66, furaha ya Kanjunju ilianza kuota mbawa, ilikuwa ni baada ya Laudit Mavugo kusawazisha kwa kichwa akiunganisha krosi ya Shiza Kichuya.

Kumbe Kanjunju alizimia baada ya bao la Mavugo, akachukuliwa kwenda kupatiwa huduma ya kwanza. Alipozinduka tayari mechi ilikuwa imefikia mwisho dakika 90 zimeisha na hakufanikiwa kuliona bao la pili la Kichuya.
Alipouliza matokeo, watu hawakuwa na hiyana, walimueleza ukweli Kanjunju kwamba Simba wameshinda 2-1 na Kichuya ndiye aliyefunga bao la pili. Safari hii Kanjunju akawa imara maana hakuzimia, akaanza kumwaga machozi na ndiyo alihojiwa na waandishi na kujulikana kwa mashabiki wengine.

Kanjunju ni shabiki wa soka kama wengine lakini ana mambo kadha wa kadha unaweza ukajifunza kupita yeye na mwisho machozi yake yakawa ni sehemu ya salamu kuwakumbusha mambo kadhaa viongozi wa soka bila ya kujali ni wa klabu gani au shirikisho.

Kanjunju huyu, anaweza kuonekana kama ni mtu asiye na fikra sahihi. Vipi mtaji wake wa biashara anaamua ‘kubeti’ akiwaamini Yanga? Ni kitu kinachoshangaza lakini lazima viongozi wajue kupitia machozi ya Kanjunju kuna watu wana mapenzi makubwa na timu zao.

Kanjunju anaiamini sana Yanga, kuamini kwake haiwezi kuwa anamuamini Mwenyekiti Yusuf Manji pekee. Badala yake analiamini benchi la ufundi pia wachezaji ambao ndiyo wanaocheza uwanjani.

Imani ya mashabiki kwenu viongozi, makocha na wachezaji ni kubwa sana. Mtu anayewekeza mtaji wake kwa imani kwenu maana yake anawaamini sana na anawachukulia kama watu wanaothamini wanachokitumikia.

Maana yake mliopata nafasi ya kuitumikia Yanga au klabu nyingine iwe Simba na kadhalika, hakika mnapaswa kuijua thamani hiyo kuwa mmebeba mioyo ya kina Kanjunju wengi wakiwemo wale wanaopoteza maisha yao.

Wanawekeza uhakika wa maisha yao, yaani mtaji kwa kuwa wanawaamini. Je, wachezaji au makocha wanajua kuna watu wako tayari kwa hilo kutokana na wanavyowaamini? Kanjunju anaiamini Yanga akijua ina watu sahihi na wanaofanya kazi kwa weledi, mapenzi na juhudi kubwa. Je, ni kweli mliopata nafasi hiyo mnaitumikia hivyo?

Kanjunju alizimia, si jambo la mzaha. Lakini mtu mzima alimwaga machozi mbele ya hadhara bila ya woga. Vizuri kila anayeguswa na hili hasa kwa wachezaji, makocha na viongozi wajue hizi klabu zenye mashabiki wengi, zinaumiza mioyo na hisia za watu.

Kufungwa ni lazima, lakini ukifungwa huku unaonekana ulikuwa unapigana. Hakuna atakayekulaumu. Hali ya kujituma au juhudi za wazi zisiwe kwenye Yanga au Simba pekee, kila mwenye sehemu yake ya kazi lazima afanye juhudi akijua kuna sehemu watu wanamuamini.

Tokea zaidi ya miaka 17 niliyoanza uandishi wa habari, sijapunguza juhudi, ubunifu na sijawahi kuchoka kwa kuwa najua nina watu wanaoniamini na sipendi kuwaangusha hata kama mimi ni binadamu, si mkamilifu.

Si vizuri kama alivyofanya Kanjunju ‘kubeti’ mtaji wake. Lakini ni vizuri kuwaamini watu wako ukiamini katika soka kufungwa kupo. Lakini narudia kusisitiza, wanaopata nafasi wakijua nyuma yao kuna watu, wayathamini mapenzi yao na hii iwafikie hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwamba watu wanaupenda mpira na wanaumia sana hivyo, utendaji wao usijali ubinafsi zaidi na hasa kwa ajili yao. Iwe kwa ajili ya Watanzania, maana kina Kanjunju wako wengi.


1 COMMENTS:

  1. Abeti tena mechi na azam...ndipo atajua kuwa hii ni awamu ya tano ya kusoma namba tu

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV