March 15, 2017
Na Mwandishi Wetu
FEBRUARI 25 watani wa jadi, Simba na Yanga walikutana kwa mara ya pili ndani ya msimu wa mwaka huu wa Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Taifa chini ya mfumo wa tiketi za kieletroniki unaoendeshwa na kampuni ya Selcom.

Ukiacha matokeo ya mchezo huo na matarajio mbalimbali ya wapenda soka waliofurika siku hiyo, kwa mara nyingine, mechi hiyo ilidhihirisha kwamba sasa hakuna kurudi nyuma katika kuendesha zoezi la mashabiki kuingia uwanjani wakitumia kadi za kieletroniki za Selcom.

Meneja Miradi wa Selcom Gallus Runyeta, ameeleza kufurahishwa na jinsi wapenzi wa soka walivyoupokea mfumo huo akisema kwamba kama ilivyokuwa kwa mechi ya kwanza ya Simba na Yanga, Oktoba Mosi mwaka jana, safari hii pia mafanikio yalikuwa makubwa.

“ Selcom kwa mara ya pili mfululizo imepata mafanikio makubwa katika fursa ya kuendesha mfumo wa tiketi za kieletroniki kwa kutumia mfumo maalum wa mageti ya umeme yanayofunguka kwa kadi maalum zenye tiketi za kieletroniki kwenye mechi zinazohusisha timu kubwa za Simba na Yanga.“ Kwa kiasi kikubwa mfumo umeweza tena kudhibiti mapato ambayo yamekuwa yakionekana kila tiketi inaponunuliwa kupitia kwa mawakala wa Selcom Tanzania nchini kote au kwa shabiki kujinunulia tiketi kwa kupitia simu yake ya mkononi.

“Mfumo una uwezo wa kutunza kumbukumbu kwa kila mtu aliyenunua tiketi na unadhibiti watu wanaoingia kwenye Uwanja kwa zaidi ya asilimia 99.99,” amesema Runyeta katika ripoti yake juu ya mchezo huo wa Simba na Yanga wa mwishoni mwa Februari 2017.

Kwa mujibu wa Meneja Miradi huyo wa Selcom, pamoja na kwamba siku hiyo ya pambano hilo la vigogo hao wa soka nchini ilinyesha mvua iliyowakwaza wengi kuweza kufika Uwanja wa Taifa, bado idadi ya wapenzi walioingia uwanjani ilikuwa kubwa ikilinganishwa na hali ya hewa ilivyokuwa tangu asubuhi.

MASHABIKI TAIFA STARS


Anasema Runyeta: “ Jumla ya watazamaji 38,705, waliingia uwanjani kupitia majukwaa ya VIP na mengineyo na jumla ya mapato yaliyopatikana ni milioni 324,810,000/ kama si hali ya hewa kuchafuka mapema kwa hamasa ya mechi hiyo ilivyokuwa matarajio yalikuwa ni Uwanja kufurika kabisa.”

Kwa mujibu wa Runyeta Selcom imekuwa ikijifunza vyema katika kukabiliana na changamoto za nyakati za kuingia uwanjani, na kuhakiki tiketi kwa ajili hiyo katika mechi iliyopita ilirahisisha zoezi zima kwa kuongeza tiketi za mfumo wa QR Code ambazo zina ufanisi sawa sawa na wa kadi za kawaida.

Anasema Selcom imewekeza katika mfumo wa utambuzi wa QR Code ili kuwawezesha wanaokwenda uwanjani ambao hawana uwezo wa kununua kadi waweze kupewa tiketi za matumizi ya mara moja papo kwa papo.

“ Hiyo ni sehemu ya zoezi zima la kuongeza wigo wa kujumuisha tiketi mbalimbali katika mfumo wa tiketi za kieletroniki kwa matumizi ya mara kwa mara katika Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru.

Kwenda mbele Runyeta anasema Selcom itaendelea kutoa elimu kwa wapenzi wa soka nchini ambao watakuwa ama wamesahau au ambao ni mara yao ya kwanza kutumia mfumo wa tiketi za kieletroniki kwa kushirikana kwa karibu na Shirikisho la Soka (TFF), sekta mbalimbali za serikali na wadau wote katika kuhakikisha kuwa elimu inawafikia walengwa.


Mfumo wa ‘wafiti’ Chamazi
Katika hatua nyingine mfumo huo umeonekana kuanza vyema kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, baada ya kutumika na kufanya vizuri katika mchezo wa Shirikisho la Afrika, uliokutanisha wenyeji Azam dhidi ya Mbambane Swallows ya Swaziland.

MASHABIKI SIMBA
Uwanja huo ambao awali ulikuwa ukiingiza mashabiki kwa kutumia tiketi za vishina, Jumapili iliyopita ulitumia tiketi za kieletroniki na mashabiki waliohudhuria uwanjani kuifurahia huduma hiyo na kuipongeza serikali kwa kuupanua mfumo huo hadi kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Kabla mfumo huo wa kisasa unaotumika kwenye Uwanja Taifa na Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, haukuwahi kutumika kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi tangu ulipoanzishwa, lakini ulivyotumika katika mchezo huo wa Shirikisho, umefanya vizuri na uongozi wa timu hiyo unafikiria jinsi ya kuendelea kuutumia katika michuano yake mingine.


Baadhi ya mashabiki waliohudhuria uwanjani hapo walisema mfumo huo ni mzuri na haukuwa na usumbufu wowote wa kuingia uwanjani kutokana na mashine kuwa nyingi na kupunguza msongamano wa mashabiki kwenye mageti ya kuingilia.

MASHABIKI YANGA


Nuhu Sadiki shabiki wa soka aliyeingia uwanjani kutumia mfumo huo alisema mfumo huo wa kisasa ni mzuri na wa kuungwa mkono ili timu ziweze kuendelea kimaendeleo.


“Mfumo huu hauna shida kama ukiwa na mashine nyingi kama ilivyo leo (Jumapili iliyopita). Tumeingia uwanjani katika hali nzuri na hakukuwa na msongamano milangoni na kila mtu aliingia kwa utaratibu mzuri ambao umewekwa na na shauri utaratibu huu uwekwe na Uwanja Taifa ili mashabiki wasiwe wanalalamika.

Uongozi wa Azam umesema mfumo huo umekuwa rafiki kwao kutokana na kukatwa fedha kutokana na idadi ya mashabiki tofauti na tiketi za vishina ambazo wakizinunua ndiyo inakuwa mzigo wao tayari na haijalishi kama wameuza tiketi zote walizozinunua au la.


Ofisa Habari wa timu hiyo Jaffar Iddi alisema kupitia tathimini fupi walioiona kwenye mchezo wao huo wataenda kukutana kama uongozi na kujua ni jinsi gani ya kuweza kuutumia mfumo huo wa kisasa kabisa.


“Kama timu tumeukubali mfumo huu ambao hautubani katika masuala ya tiketi. Mara nyingi tumekuwa tukinunua tiketi kwa wauzaji na kuja kuziuza kwa mashabiki na tukitaraji kupata faida kupitia mauzo yetu kwa mashabiki lakini wakati mwingine tunapata hasara kwa kununua tiketi nyingi na kuuza chache. Lakini mfumo huu unalipwa vile ambavyo mashabiki wameingia uwanjani,” alisema Iddi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV