March 8, 2017



Huku wakiwa wanajiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco ya Zambia, uongozi wa Yanga umesema wala hawana hofu huku ukipanga kuwatumia Obrey Chirwa na Justine Zullu wanaotoka nchi moja na wapinzani wao.


Kauli hiyo, ameitoa Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa baada ya wapinzani wao kutotoa taarifa za ujio zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya pambano hilo.


Timu hizo, zinatarajiwa kuvaana Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki moja ijayo huko Lusaka, Zambia.

Mkwasa amesema huo usiri wanaoufanya Zanaco wala hawauhofii, kwani timu yao ina wachezaji na makocha, George Lwandamina na Noel Mwandila waliokuwa wanaifundisha Zesco inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia.

Mkwasa alisema, anaamini kabisa kwa kupitia wachezaji wao, Chirwa na Zullu watazipata mbinu wanazozitumia wapinzani wao katika mechi hiyo.

Aliongeza kuwa, hadi hivi sasa hawajapata taarifa ya ujio wao kama watawalipia au kujilipia wao hoteli na huduma nyingine mara watakapotua nchini.


"Niseme tu kuwa, hadi hivi sasa uongozi wa Yanga hatujapata taarifa zozote kutoka kwa wapinzani wetu kuhusiana na tarehe ya kutua nchini, labda kitu kikubwa nitakachokisema ni kuwa sisi tumejiandaa kupata ushindi kwenye mechi hii ya nyumbani.

"Na kwa kuwatumia wachezaji wetu, Chirwa na Zullu, pia benchi letu la ufundi chini ya Lwandamina na msaidizi wake Mwandila wote wanaotokea nchini Zambia tutapata ushindi.


"Uongozi unaamini kuwa, unawajua kabisa Zanaco na hasa wale wachezaji hatari kwa ajili ya kudhibiti mbinu zao ili kuanzia mechi ya hapa nyumbani na ugenini zote tupate ushindi," alisema Mkwasa.

A

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic