April 12, 2017


Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amemshangaa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Salum Mkemi na kumuita “mpiga kelele”.

Hans Poppe amesema Mkemi, amekuwa akipiga kelele na kuitishia kamati ya saa 72 kutofanya maamuzi sahihi kuhusiana na rufaa ambayo wamekata Simba dhidi ya Kagera Sugar, ikidai ilimchezesha beki Mohamed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano. Katika mechi hiyo Simba walilala kwa mabao 2-1.

“Unajua yule mpiga kelele wa Yanga ni mtu asiyejua mambo, asiyejua historia ya mpira. Ni mtu anayepiga kelele tu ilimradi aseme na kufurahisha genge.

“Anasema akiitaja Serengeti eti itaathirika kama suala hilo litaenda mahakamani na Fifa wataifungia Tanzania. Lakini hajui hata Serengeti imefuzu baada ya kudai haki yake kama ambavyo Simba inavyodai.

“Hapa si suala la kuitisha kamati, hapa ni data. Kagera inajulikana wamemchezesha mchezaji ana kadi tatu za njano, basi sheria ichukue mkondo wake.

“Kwa nini hili jambo linaonekana kama ni geni au limeanza kwa mara ya kwanza baada ya Simba kukata rufaa. Huyo mpiga kelele hajui kuwa Simba iliwahi kukatiwa rufaa na Kagera kwa kumchezesha Mgosi akiwa na kadi tatu za njano, ikapoteza pointi.

“Tena pointi hizo ziliisaidia Yanga kuwa bingwa baada ya Simba kupungukiwa. Sasa kama hajui vizuri anyamaze kuliko kuendelea kupiga kelele kwa mambo asiyoyajua,” alisema Han Poppe.

Mkemi alitangaza Yanga kuipa onyo kamati hiyo isiipe Simba pointi tatu kwa madai kuwa ilishindwa uwanjani hivyo haitakiwi kudai pointi za “mezani”.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic