April 19, 2017


Na Saleh Ally
SIMBA imetoka Kanda ya Ziwa na jumla ya pointi saba kati ya tisa. Hii ni baada ya kucheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara.
Mechi ya kwanza ni dhidi ya Kagera Sugar, baada ya hapo ikateremka mjini Mwanza na kucheza mechi mbili dhidi ya Mbao FC na baadaye Toto African.

Kama ingekuwa ni uwanjani, maana yake Simba ingerejea na pointi nne tu na kuwa imepoteza tano. Hii ni baada ya kufungwa na Kagera Sugar kwa mabao 2-1, lakini baadaye uongozi wake ukakata rufaa na kushinda baada ya kubainika Kagera Sugar walimchezesha beki Mohamed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano.


Walipokwenda Mwanza, wameshinda mechi dhidi ya Mbao FC kwa mabao 3-2 na mechi ya mwisho dhidi ya Toto African ilikuwa ni sare ya bila kufungana.

Nataka kukiangalia kikosi cha Simba ambacho kipo kileleni mwa Ligi Kuu Bara na kujaribu kutafakari aina ya uchezaji, wachezaji wake wenyewe na morali au ndoto ya kuichezea Simba na kupata mafanikio kama wanayo.

Katika mechi dhidi ya Kagera Sugar, pamoja na kufungwa, hakuna ubishi wenyeji walionyesha soka safi zaidi ya wageni ambao ni Simba. Wakashinda na wangeweza kushinda zaidi kama wangekuwa makini.

Simba walipokwenda Mwanza, mechi dhidi ya Mbao FC, hadi dakika ya 82 walikuwa nyuma kwa mabao mawili safi na ya kuvutia yaliyofungwa na Mbao FC ambayo ilionyesha kiwango kizuri kipindi chote cha kwanza kuzidi wao.

Simba ilianza kusawazisha mabao yake kuanzia dakika ya 83 na hili ndilo lililowasahaulisha wengi kwamba Simba ilionyesha kiwango kibovu katika mechi hiyo. Hata wakati wanafunga mabao hayo matatu, Simba hawakuwa na mpira zaidi ya mipira ya juu, “gombania goli” na mabao yakapatikana.Angalia mechi ya tatu dhidi ya Toto African ambao walionyesha kujiamini na kucheza utafikiri ndiyo Simba ambao walionekana ni waoga na inawezekana wangefungwa wakati wowote ule.

Toto African ndiyo waliopoteza nafasi nyingi za kufunga huku wachezaji wa Simba akiwemo Frederic Blagnon aliyetamba dhidi ya Mbao FC kwa kufunga mabao mawili, wakionekana hawana msaada hata kidogo.

Kama ni uwanjani, unaweza kusema wachezaji wa Simba hawakuonyesha kuwa kweli wao ni Simba, timu kongwe, kubwa yenye malengo, inayotaka kuchukua ubingwa wa Tanzania Bara baada ya kuukosa kwa misimu minne.


Jiulize, vipi wachezaji wa Kagera Sugar wanacheza vizuri zaidi, kwa juhudi zaidi kuliko wale wa Simba wanaolipwa vizuri, mazingira mazuri zaidi ya kazi na ubora wa mengi kama wachezaji wa timu kubwa!Walipokwenda kucheza na Mbao FC, ikaonekana kiwango cha Mbao FC pia ni bora zaidi yao huku wachezaji hao wa timu hiyo ya watu wanaochangishana ikitamba zaidi kuliko wao.

Wamesalimika kufungwa na Toto African ambayo wachezaji wake wanne walikuwa wamesimamishwa, wakarudishwa siku moja kabla. Mishahara hawakuwa wamelipwa na bado mishahara yao hata wakilipwa ni midogo sana.


Faida ya kuwalipa wachezaji wa Simba mishahara mikubwa, matunzo bora, fedha kubwa za usajili ni ipi kwa Simba?
Je, wanaocheza timu hiyo wanajua maana yake? Hawawezi kuonyesha kiwango bora ni kwa kuwa kiwango cha ufundishaji cha Kocha Joseph Omog hakina mbinu mbadala. Kwamba Simba wakibanwa katika kitu kimoja, hawana ujanja.

Tunajua nini maana ya kuwa na wachezaji wa kigeni. Mfano Simba katika mechi dhidi ya Toto ilianza na wageni saba. Halafu hakuna aliyeng’ara wala kuonyesha uwezo bora ambao ungekuwa gumzo.

James Kotei raia wa Ghana pekee amebaki kuwa mfano wa kuigwa. Hii inaonyesha kiasi gani wachezaji wa kigeni wanaostahili kuchezea katika timu zetu.


Katika ushindani bora, wanapaswa kuwa washindani wa kweli. Ambako ushindani uko chini, waonyeshe ubora zaidi na kuwa changamoto kwa wazawa.

Lakini hata wao wazawa ni bora? Kweli wachezaji walio Simba ni bora zaidi ya walio Toto, Mbao na Kagera? Au ni kundi la watu lililojivisha Usimba na kutaka kuogopwa kumbe halina tofauti na kwingine.

Wanaweza kufungwa, lakini kiwango chao cha ubora kilikuwaje? Wanaweza kushinda au kupata sare, lakini kweli walionyesha ni bora, sahihi na washindani wanaopaswa kuwa mfano?


Hakika Simba haina uwezo wa kuonyesha kuwa ni timu imara, timu ya kuogopwa au tishio. Badala yake walipokutana na timu za Kanda ya Ziwa, walionekana ni timu ya kawaida na iliyopaswa kuogopa na si kuogopwa.


Kuna haja ya kujifunza kwa wachezaji wa Simba kupitia Kanda ya Ziwa. Kuvaa jezi tu ya Simba haitoshi badala yake wanapaswa kujua thamani na kwa nini wako hapo. Mechi tatu zilizobaki, zitatoa majibu na huenda itakuwa nafasi nyingine ya kuamsha au kufungua mjadala huu.

SOURCE: CHAMPIONI


8 COMMENTS:

 1. Mkuu unakosea sana kwa Kufananisha viwango vya wachezaji wa Simba na toto afrc,mbao na kagera sugar fc, Umesahau ni kwa jinsi gani Timu za Simba,Yanga na Azam zinapata shida sana kupata point 3,zinakwazwa na mambo makuu matatu, Hali ya hewa,Viwanja na Ushirikina wa kutisha.Mfano mechi ya Simba na Mbao kichuya aliwaokoa Simba baada ya kwenda kuondoa ndumba golini mwa Mbao na kuitupilia mbali dk za lala salama baada kutoa ile ndumba Simba walipata matokeo mazuri.Je unataka kujifanya haya mambo ya ushirikina huyajui.Umesahau hizo timu zimecheza mzunguko wa kwanza dar zimefungwa zote.Kifupi Timu za mikoani hazina ubunifu wowote zaidi ya kucheza kwa kukamia na kuharibu burudani uwanjani.Angalia mechi za wao kwa wao zinacheza chini ya kiwamgo wanacheza kama mpira wa ndondo.

  ReplyDelete
  Replies
  1. hii ni aibu kwa mwanamichezo kuzungumzia ushirikina kwenye mpira, labda ni wapi timu ilishinda kwa kigezo cha ushirikina bila kufanya mazoezi na kuwa na mbinu za ushindi uwanjani? Simba na Yanga hazina hata viwanja vya kufanyia mazoezi, kutoa sababu kama hii ni kukosa vision ya maendeleo....Umesahau kiwango kikubwa walichokionesha Mbao pale taifa na kuwalazimu kupata matokeo dakika za lala salama? kwangu mimi wachezaji wa kigeni mchango wao ni mdogo ukilinganisha na mishahara mikubwa wanayochukua..... Mwandishi wa story hii yuko sahihi.... Mbao,Kagera sugar na Toto Africans walikuwa bora zaidi kuliko Simba.

   Delete
 2. Kabisa mkuu simba naona lile tatizo la arsenal la kushindwa kumaliza mbio linawakumba.. Yani wanacheza utafikiri timu ya daraja la pili..wanatuboa sana ss mashabiki

  ReplyDelete
 3. Aliyeandika hiyo makala nadhani alipaswa kuwa fare, Yanga, Azam zina wachezaji wengi wa kigeni, unataka kuniambia Yanga haijawahi kupoteza mechi? Azam ipo wapi pamoja na kuwa na wachezaji wa kigeni? Nadhani wewe si mchambuzi mzuri wa soka na hujui soka zaidi ya ushabiki usio na mashiko.

  ReplyDelete
  Replies
  1. This comment has been removed by the author.

   Delete
  2. Na pia hizo alizozitaja huwa zinakamia sana mechi maana wangecheza mechi zote jinsi wanavyocheza na simba wasingekuwa nafasi walizopo

   Delete
 4. Mwandishi, naona ulitulia na dawa ikakuingia vilivyo.

  ReplyDelete
 5. huu ndo ushabiki sio uandishi na uchambuzi wa habari za michezo coz siku zote mchambuzi unatakiwa kuwa na weledi na pia netral hata kama timu unayoichambua huipendi, hutakiwi kuonyesha chuki. Mfano juzi tu Team tunayoishabikia wengi ya Chelsea imefungwa nyumbani na Crystal palace unataka kutuambia wachezaji wa Chelsea hawakuwa na morali ya ushindi? ama hawajitambui thamani yao? huo ni ushabiki sio uchambuzi mchezo wa mpira una matokeo matatu.

  ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV