Kocha wa Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon ameweka bayana kwamba mipango yake haijaharibika kabisa baada ya kuambulia pointi saba badala ya tisa ambazo walikuwa wanazitegemea kuzivuna kwenye michezo yao ya Kanda ya Ziwa, ambapo kwa sasa mikakati yake iliyobakia ni kuhakikisha wanaibuka na pointi zote katika michezo mitatu watakayocheza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ambayo ina jumla ya dakika 270.
Juzi Jumamosi Simba ilimaliza michezo yake ya Kanda ya Ziwa kwa kucheza na Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambapo timu hizo hazikufungana.
Kwenye mechi nyingine za ukanda huo Simba iliwafunga Mbao FC mabao 3-2 na kupewa pointi za Kagera Sugar licha ya kufungwa mabao 2-1 baada ya kumkatia rufaa beki Mohammed Fakhi ambaye alikuwa na kadi tatu za njano.
Omog alisema licha ya kutofanikiwa kwa malengo ya kuchukua pointi tisa kutoka kwa Toto, Mbao na Kagera lakini pointi ambazo wameambulia zitaweza kuwasaidia kwenye kampeni yao ya kuchukua ubingwa.
“Siyo vibaya kwamba tumepata pointi saba badala ya tisa kama tulivyopanga awali, nasema hivyo kwa sababu ni bora tumeambulia pointi hizo kuliko tungefungwa kabisa kwani ingetutoa kwenye mbio za kugombania ubingwa.
“Ni ngumu kupata pointi hizo kwenye michezo hii ya mwishoni kwa sababu kila timu inakuwa inajipanga kikamilifu kuhakikisha haipotezi kirahisi ili kujiepusha na suala la kushuka daraja.
“Tulichokibakisha kwa sasa ni kupata matokeo mazuri kwenye mechi hizi zilizobaki ambazo tutakuwa na faida ya kucheza katika uwanja wa nyumbani na nina uhakika kwamba hatutakuwa na cha kupoteza kwa sababu lengo ni kupata pointi zote katika michezo hiyo,”alisema Omog.
Simba kwa sasa imebakisha michezo mitatu pekee ambayo yote wataicheza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar dhidi ya Mwadui FC na Stand United za Shinyanga pamoja na African Lyon.
0 COMMENTS:
Post a Comment