MBARAKA |
Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, raia wa Cameroon, ameibuka na kumchambua straika Mbaraka Yusuph wa Kagera Sugar kwa kusema kuwa mshambuliaji huyo ni hatari kwani aliweza kuichachafya ngome yake iliyokuwa mikononi mwa Mganda, Juuko Murshid.
Kagera iliyokuwa nyumbani katika Uwanja wa Kaitaba, Kagera wikiendi iliyopita ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba ambapo Mbaraka alifanikiwa kufunga bao moja kati ya hayo. Bao lingine lilifungwa na Edward Christopher ‘Eddo’.
OMOG |
Omog amesema kwamba Mbaraka ni miongoni mwa mastraika hatari kwa sasa na hilo linadhihirishwa na kiwango chake cha kufunga mabao lakini pia kutoogopa mabeki na upambanaji.
“Ni mshambuliaji mzuri na anayejua kufunga, nimpongeze juu ya hilo lakini pia nimebaini kwamba ana kiu ya kupambana na haogopi beki yeyote yule na katika mechi yetu na wao yeye pamoja na kipa Juma Kaseja ndio waliotubania kuibuka na pointi tatu.
“Utaona kipaji chake kwa jinsi alivyoivuruga beki yetu ambayo ina wachezaji wazuri lakini walimshindwa na alitufunga, jambo ambalo naweza kusema kwamba ni mchezaji hatari na kama akiendelea kudumu katika kiwango chake atafika mbali,” alisema.
Katika hatua nyingine, bosi huyo wa benchi la ufundi la Simba, amezungumzia suala la ubingwa ambao amesema licha ya kupoteza mechi na Kagera lakini wana matumaini makubwa ya kuutwaa kwa msimu huu.
“Kupoteza mechi ni suala la kawaida na ndiyo matokeo yanayopatikana uwanjani, lakini niwatoe hofu kabisa mashabiki kuwa hapa tumeteleza na hatujaanguka hivyo tunajipanga kwa ajili ya mechi zinazokuja na imani yetu tutashinda zote,” alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment