Na Saleh Ally
JUMATANO iliyopita, mshambuliaji nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo alikwenda uwanjani jijini Munich, Ujerumani akiwa na mabao 98 ya Ligi ya Mabingwa na michuano mingine ya Ulaya kwa upande wa klabu.
Ronaldo raia wa Ureno, alimaliza mechi hiyo akiwa ameisaidia Madrid kuishinda Bayern kwa mabao 2-1 licha ya kwamba walikuwa nyumbani. Alikuwa ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza barani Ulaya kufunga mabao 100 kwa ngazi ya klabu.
Ronaldo aliweka rekodi hiyo mpya, kwanza akimpiku Lionel Messi ambaye siku moja kabla aliingia uwanjani akiwa na mabao 97 ya Ulaya. Barcelona ikaambulia kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Juventus, naye akatoka na mabao hayo 97 tena.
Ukiachana na Messi, kuna wakongwe wengine ambao wamestaafu kama Raul Gonzalez mwenye mabao 76 hadi anastaafu baada ya kufanya vizuri akiwa na Madrid na baadaye Schalke 04 ya Ujerumani.
Wako kama Filippo Inzaghi aliyestaafu na mabao 70 huku akiipa AC Milan mafanikio makubwa kama ilivyokuwa kwa Andriy Shevchenko aliyekuwa na mabao 67. Wachezaji wa miaka ya 1990 au 1980 ni Mjerumani pekee, Gerd Muller aliyefikisha mabao 70.
Hii peke yake inakufanya uone, Ronaldo si mtu wa kawaida na mabao yake 100 usiyachulie kama hadithi pekee kwa kuwa hayawezi kupatikana kwa urahisi tena kwa mtu aliyeibuka hivi karibuni ukilinganisha na wengi.
Mchezaji mwenye rekodi lukuki na hakuna ubishi, Ronaldo si mchezaji mnyumbulifu ambaye kwa maana ya kipaji unaweza kumfananisha na mtu kama Messi, ni mwenye juhudi ya kiwango cha juu, anayetaka kushinda na uthubutu wa juu kabisa.
Ronaldo alitua Manchester United mwaka 2003 akitokea Sporting Lisbon ambayo katika mechi 25 alikuwa amefunga mabao matatu tu. Alikuwa mchezaji kinda na asiye na jina na Man United walimchukua baada ya Kocha Sir. Alex Ferguson kumuona kwenye mechi ya kirafiki kati ya Man United na Sporting Lisbon waliyoshinda mabao 3-1.
Misimu sita akiwa Man United alipata mafanikio makubwa ni pamoja na kuwa mwanasoka bora wa dunia, akaipa ubingwa wa England, ubingwa wa Ulaya, ubingwa wa dunia na yeye kuwa mwanasoka bora wa dunia. Jumla alicheza mechi 196 na kufunga mabao 84.
Alipohamia Madrid mwaka 2009, alionekana ni nyota hasa, lakini sasa ni nyota kwelikweli na kiwango chake kilipaa kwa kasi ya kimondo, amecheza mechi 260 na kufunga mabao 279!
Amebeba ubingwa wa La Liga, Copa del Rey, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Uefa Super Cup, Kombe la Dunia la Klabu na amekuwa mwanasoka bora duniani mara tatu. Jiulize huyu ni mtu wa namna gani?
Si rahisi au itashangaza kama utamuona Mreno huyo ni mtu wa kawaida tu na alipofikia ni suala la hadithi na linapaswa kupita linaonekana limepita.
Kipaji anacho, lakini alivyo inaonyesha si cha kutisha kupitiliza na huenda wako wengi wenye soka la kuvutia na burudani lakini wameshindwa kufikia mafanikio kwa maana ya mtu anayetaka kushinda, anayetaka kufika anakotaka na kufanikiwa.
Ronaldo ni mtoto anayetokea katika familia masikini, baba yake mzazi alikuwa mtumishi na mtengeneza bustani. Anaijua shida, anayajua mateso yake na anatokea katika familia duni katika Kisiwa cha Madeira nchini Ureno ambacho hivi karibuni, serikali yake imeamua kuupa jina la Uwanja wa Ndege wa Madeira kuwa uwanja wa Ronaldo.
Mafanikio anayoyapata Ronaldo ambaye sasa ni milionea anayemiliki hoteli katika miji mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kuingiza mamilioni ya fedha kutokana na mikataba yake minono, inaonyesha hakuna mambo ya ujanja badala yake, kazi kwa juhudi na maarifa ni namba moja.
Ronaldo huonekana kama “brothermen” Fulani, lakini uhalisia unaonyesha ni kijana anayejituma, anayejua anataka nini na huenda fedha inafuatia kwani ni anayetaka mafanikio.
Wakati akiwa Man United, katika moja ya vitabu vyake, Wayne Rooney aliwahi kuandika kwamba hakuwahi kufika mazoezini baada ya Ronaldo kwa kuwa alikuwa akimkuta mazoezini kila anapofika.
Mara nyingi, Ronaldo ndiye alikuwa wa mwisho kuondoka mazoezini. Jambo ambalo linaonyesha ni aliyepania kufanikiwa na anataka kupita njia sahihi ili kufikia anachohitaji.
Hadithi ya mabao yake 100, inaweza kuchukuliwa kama jambo dogo na la kawaida sana. Kila anayewaza hivyo lazima ajifikirie mtu aliyetokea sehemu duni nchini Ureno, akaenda kung’ara katika ushindani wa ligi bora za England na Hispania na sasa ndiye bora zaidi, si jambo dogo.
Kwako Mtanzania, si rahisi kuwa kama Ronaldo lakini misingi na njia za Ronaldo zinaweza kuwa sehemu ya kukuhamasisha kwamba kuna jambo ulilotaka kufanikiwa, huenda umekatishwa tamaa, basi usihofu, amka tena.
Inawezekana una uwezo, lakini wapinzani wako wamekuwa wakijaribu kukukatisha tamaa na kukurudisha nyuma. Badilika, jitambue na uamke, anza kufanya kilicho sahihi.
Mabao 100 ya Ronaldo yanaonyesha hakuna anayeweza kuzuia ndoto zako kama wewe ndiye utakuwa umeamua. Lazima upende ndoto zako halafu ufanye kazi kwa juhudi na maarifa na kujiamini unaweza kufikia.
Mbwana Samatta yupo njiani kufikia ndoto zake baada ya kutoka DR Congo na kwenda Ubelgiji ambako wote tunaona anafanya vizuri. Je, wewe unajiandaa kwenda wapi? Unataka kuishindia Simba na Azam FC pekee ndiyo panakutosha?
TAKWIMU ZA RONALDO:
WAFUNGAJI BORA ULAYA:
MABAO MECHI
Cristiano Ronaldo 100 143
Lionel Messi 97 118
Raul Gonzalez 76 158
MGAWANYO MABAO 100 YA RONALDO:
Ligi ya Mabingwa 97 136
Uefa Super Cup 2 1
Kufuzu Ligi ya Mabingwa 1 3
NCHI AMBAZO AMEFUNGA MABAO MENGI:
Ujerumani 20
Italia 13
England 9
Ufaransa 9
MABAO ALIYOWAFUNGA WAPINZANI:
MABAO MECHI
Schalke 7 4
Ajax 7 5
Malmo 6 6
Bayern 6 5
Galatasaray 6 3
KATIKA MABAO YAKE 100…
AMEFUNGA…
16 akiwa na Man United
84 akiwa na Real Madrid
Mabao 2 au brace mara 26
Mabao 3 au hat trick mara 5
0 COMMENTS:
Post a Comment