April 19, 2017Uongozi wa Yanga kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Clement Sanga, umewapiga ‘stop’ wachezaji wa timu hiyo kuzungumzia masuala ya kadi tatu za njano yanayomhusu beki wa Kagera Sugar  Mohammed Fakhi.


Fakhi alikatiwa rufaa na Simba kwa kile kinachodaiwa kuwa aliichezea timu yake ya Kagera akiwa na kadi tatu za njano mchezo ambao Kagera walipata ushindi wa mabao 2-1.

Hata hivyo, baadaye Kamati ya Masaa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania TFF iliipa Simba ushindi kwenye mchezo huo, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na mashabiki wa soka nchini.

Uongozi wa Yanga wenyewe umesema kuwa hautaki kuwaona wachezaji wao wakijadili kuhusu kadi hizo bali waendelee kupambana uwanjani kwani wakishinda michezo yao yote bado wanaweza kuwa mabingwa.

Sanga alisema kuwa haoni sababu ya Msuva au mchezaji yoyote wa Yanga kwa kipindi h kujadili mambo ya Simba na Kagera Sugar wakati mambo hayo si ya Yanga bali ni ya kamati za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na walalamikaji husika.

“Kweli kwa sisi tusingependa sana kwa kipindi hiki kumuona mchezaji yoyote wa Yanga akitumia muda wake mwingi kuwazia mambo ya kadi tatu za Fakhi au kuanza kulijadili suala hilo.


“Maana tungependa kuelekeza mawazo na akili zetu katika michezo iliyosalia, kwani matokeo yanaweza kupatikana uwanjani tu na siyo sehemu nyingine,” alisema Sanga.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV