April 5, 2017Na Saleh Ally
WAKATI Yanga inafanikiwa kuifunga Azam FC kwa bao 1-0 wiki iliyopita, huenda kila kitu kingekuwa rahisi kama ungeangalia kwa jicho la kawaida.

Lakini mambo mengi yalijitokeza ambayo yanakuwa somo kuu kwa mchezo wa soka na huenda mechi hiyo inaweza kutumika katika mambo mengi kama ushabiki utakaa pembeni kwanza.

Yanga iliingia uwanjani ikiwakosa wachezaji takribani watano kati ya wale iliokuwa ikiwategemea katika kikosi cha kwanza na Wanayanga wengi walijawa hofu na kuona kama tayari walishapoteza mechi hiyo na ushindi kwao ingekuwa sare.


Mpira unapendwa kwa kuwa unaamua matokeo yake wenyewe na si nani anaamini, kutabiri au kuona. Kama unakumbuka Azam FC walitawala kila idara, mwisho waliofanya kweli walikuwa ni Yanga.

Yanga waliwakosa Donald Ngoma, Amissi Tambwe ambao wanawategemea kwa ufungaji. Kelvin Yondani aliyekuwa na kadi na Thabani Kamusoko ambaye ni majeruhi.


Pia walikuwa wanamkosa beki wa kulia, Hassan Kessy ambaye sasa ni tegemeo katika ulinzi upande wa kulia. Hivyo akacheza Juma Abdul ambaye hakuwa amecheza mechi kadhaa.

Yanga walipata bao katika dakika ya 70, mfungaji akiwa Obrey Chirwa ambaye alipokea pasi ndefu kutoka mbele kidogo ya lango la Yanga lakini akatoka kasi na kuuwahi mpira.

Chirwa alikuwa msaada mkubwa katika kusoma mawazo ya mtoa pasi, Haruna Niyonzima ambaye alipiga mpira huo pia baada ya kumsoma mfungaji akiamini mambo kadhaa.Kuwa ana kasi, mpira mrefu kama ule angeufikia na suala la umaliziaji angemuachia mwenyewe achague na Mzambia huyo aliweza kuumiliki mpira, akaingia kwenye boksi, akatulia na mwisho akafanya moja ya umaliziaji bora kabisa.


Kama uliona Yanga walivyokuwa wakicheza kwa tahadhari kubwa, walionyesha ukongwe ni dawa kuhakikisha Azam FC hawasababishi madhara langoni mwao hata kama watashambulia vipi.


Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye Yanga walianza kumdharau na kumvisha uzee kisa Vincent Bossou kuanza kumuweka benchi, nafikiri wanapaswa kukumbuka na kufikiri mara mbili.

Nikirudi kwenye pasi ya Niyonzima raia wa Rwanda ambayo ilimaliza mchezo, unagundua Niyonzima ni mchezaji wa aina tofauti sana kama utalinganisha na wachezaji wengi tulionao.
Kushindana na Niyonzima kama mchezaji ni vizuri lakini wachezaji wa hapa nyumbani wasimuache aondoke wakiwa hawajajifunza lolote kutoka kwake.Angalia kabla ya pasi hiyo, karibu kila mpira alipewa yeye auanzishe. Alijua wakati wa kupeleka haraka na wakati wa kutuliza mambo.

Baada ya pale alikuwa na jicho zaidi ya lile la tai au wale mwewe wakubwa.  Anajua mpira uende wapi kulingana na mazingira na muda.

Kwa anachofanya Niyonzima anakuwa mtu mmoja anayecheza nafasi ya watu zaidi ya wawili. Anakuwa kocha kwa kupanga mipango ya ndani lakini ni kiungo anayekaba na kupeleka mashambulizi.

Pasi yake iliyomaliza mchezo ilihitaji ubora wa juu kabisa kwa kuwa unatakiwa kuangalia itakwenda wapi, kupima kama mtu atafika kwa wakati mwafaka na wakati wa kuipiga hakikisha inafika kama ilivyotakiwa.


Niyonzima hana papara, si mtu mwoga kujaribu anachotaka kufanya na si mwoga kukosea. Kwa wale wanaoangalia mechi ngumu za Yanga, watakuwa na nafasi ya kujua ubora wake.Timu inapokuwa imezidiwa, Niyonzima haonekani kwa matukio muhimu kama hilo la utengenezaji bao lakini siku Yanga ikishinda, basi utamuona katika uburudishaji kwa maana ya kutoa pasi za uhakika, au “kuwaharibu” wapinzani kisaikolojia.

Niyonzima ni kati ya viungo bora kabisa ambao Yanga imewahi kupata na mashabiki wanapaswa kuonyesha heshima kwake leo badala ya zile habari za mtaani ambazo zinasababisha wao kusema maneno mengi ya dharau dhidi yake.


Kuna kila sababu ya kujifunza, kukubali kazi na ubora wa watu fulani kwa wakati mwafaka badala ya kusubiri wakiondoka, basi sifa ziwe nyingi kama ambavyo Wabunge walivyomshangilia Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, kama walikuwa ndiyo wanamuona kwa mara ya kwanza hiyo jana.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV