April 28, 2017




Na Saleh Ally
LILE sakata la rufaa za Simba na baadaye Kagera Sugar limeisha kwa Kagera Sugar kurejeshewa pointi zao tatu.
Nikukumbushe kidogo, Simba ilichapwa kwa mabao 2-1 na Kagera Sugar, baada ya mechi hiyo Simba wakakata rufaa kwamba beki wa kati wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi, alikuwa na kadi tatu za njano na Kamati ya Saa 72 ikakaa na kuipa Simba pointi tatu baada ya kubaini alikuwa nazo kweli.


Hapo Yanga ambao ni wapinzani wakubwa wa Simba, waliibuka na kuanza kupambana wakisema hilo halitawezekana na wangetaka kuona pointi tatu za Kagera Sugar ambao walishinda uwanjani zinarejeshwa.


Kagera Sugar wakakata rufaa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ikakutana mara ya kwanza na kufanya mahojiano na watu mbalimbali, ikafanya hivyo mara nyingine kuwahoji wengi wakiwemo waamuzi, mchezaji mwenyewe, viongozi, hadi aliyedaiwa kusababisha kadi.


Baada ya hapo ulitolewa uamuzi kwamba pointi zingerejea Kagera Sugar. Wakati kamati hiyo ikitoa uamuzi, hakukuwa na maelezo kama kweli ilibainika Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano au la.

Ukweli ni kwamba hadi leo, TFF haijasema, kamati iliyoamua haijasema, kama kweli ana kadi tatu za njano au mbili. Hata ile kamati ya nidhamu ambayo ilimhukumu Haji Manara nayo haikulizungumzia suala hilo hata kidogo kwa kuwa kauli zilizomfunga Manara, zilihusiana na suala hilo la kadi.

Bado nashindwa kusimamia upande wowote kwa kusema kweli Fakhi alikuwa na kadi tatu, hivyo Simba ndiyo walikuwa ni wenye haki. Lakini vigumu pia kusema Kagera walipaswa kurudishiwa pointi kwa kuwa Fakhi hakuwa na kadi mbili.

Simba wanasema alikuwa na tatu, Kagera wanasema alikuwa na mbili na hadi sasa suala hilo linabaki lilivyo kwa kuwa aliyepaswa kuuthibitishia umma wa Watanzania ni TFF kwa kuwa ndiyo inatakiwa kunajua.

Kama nilivyowahi kueleza TFF pamoja na Bodi ya Ligi ndiyo wakusanya rekodi, pia wahifadhi rekodi. Sasa hadi sakata hili linaisha, hakuna anayejua kama Fakhi ana kadi mbili za njano au tatu!

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imeliruka suala la kadi tatu au mbili za njano. Ikakimbilia kwenye kusema Simba haikuwa imefuata utaratibu sahihi katika ukataji wa rufaa, hivyo inaonekana rufaa yake haikupaswa kusikilizwa.

Wako sahihi kabisa, Simba walipaswa kufuata utaratibu. Lakini rufaa kutofuata utaratibu, bado haiizuii kukamilika kwa kosa kama Fakhi ana kadi tatu. Kwa kufuata kanuni za ligi, kama kuna kadi tatu na mchezaji alicheza, hilo ni kosa na halisubiri rufaa kama ambavyo Azam FC walipoteza pointi zao bila rufaa.

TFF imeshindwa kujua mchezaji kama ana kadi mbili au tatu. TFF imeshindwa kuwathibitishia kama Fakhi alikuwa na kadi mbili tu na pointi zinapaswa kubaki Kagera? Hii ni ajabu sana.

Lakini naendelea kushangazwa na TFF ambayo kamati yake moja imesema kuna kadi tatu, nyingine ikanyamaza na kutoa hukumu na TFF ikadanganya iko kimya wakati imeshindwa kuonyesha iko makini.


TFF ina tatizo, ndiyo tatizo la kukwama kwa mpira wetu na hapa wala kusiwe na kisingizio kwamba wanaolifuatilia suala hili wanataka timu fulani ipewe pointi au kupokonywa.

Kikubwa hapa ni hivi; suala hili la kadi limezidi kuonyesha TFF inayoongozwa na Jamal Malinzi imefeli. Maana kama inashindwa kupata uhakika wa kadi tu, itasaidiaje maendeleo ya mchezo huo?


Bado mimi nitaendelea kusisitiza, sitaki kuingilia uamuzi uliotolewa. Lakini nataka kujua je, Fakhi alikuwa na kadi mbili za njano, au tatu? TFF inapaswa kulisema hili na ni jukumu lao kufanya hivyo kwa kuwa wahusika akiwemo Malinzi, ni watumishi wa Watanzania kwa kuwa TFF ni ya Watanzania na si watu au kundi fulani la watu.

2 COMMENTS:

  1. Acha ubashite kijana we endelea kukusanya ushilawadu ili upakibarua kwa Erick,mambo ya Ngoswe waachie ngoswe wenyewe!Pilipili usoila yakuwashaje?

    ReplyDelete
  2. Kaka uko sahihi kwa mpenda soka na mtaka maendeleo ya soka letu lazima atakubali kuwa hoja zako zina mashiko mno,,TFF hii imefanya madudu mengi kuliko mazuri.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic