Unaweza kusema sasa kuwa hadi kieleweke kwa kuwa mwamuzi Jonesia Rukyaa ndiye aliyeingia katika chumba walicho wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Rukyaa ndiye atakuwa anahojiwa kwa sasa kwa kuwa alikuwa mwamuzi katika mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Kagera Sugar na African Lyon. Na taarifa zinaeleza amesema Fakhi hakupigwa kadi ya njano!
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa waamuzi ambaye ni mtu wa karibu wa Jonesia, amesema kuhusu mwamuzi huyo kusema yanayoelezwa, ni uzushi kwa kuwa hata kabla hajaingia kuhojiwa, tayari kuna taarifa zilishaanza kuandikwa mtandaoni.
Awali kumekuwa na taarifa kwamba mwamuzi huyo hakuiona kadi hiyo, lakini baadhi ya watu wa Simba walimtuhumu kupangwa 'kutumika' aikatea kadi.
Hata hivyo, Jonesia ndiyo yuko kikaoni na haijajulikana alichosema ukiachana na maneno hayo ya hisia kwamba atasema nini.
Kikao hicho kinafanyika katika hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam na uongozi wake umezuia makomandoo wa Yanga na Simba kuingia katika eneo hilo.
Tayari maofisa wa Kagera Sugar pia Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' waliingia kuhojiwa.
Baada ya hapo, kikao hicho kimekuwa kikiendelea na huenda baada ya saa moja au mawili kinaweza kufikia tamati.
Kagera Sugar wamepinga Simba kupewa ponti tatu na mabao matatu kupitia Kamati ya Saa 72 iliyobaini beki Mohamed Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano.
Tayari imeelezwa majibu yatatolewa leo saa 11, lakini tayari zaidi ya saa moja sasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment