April 17, 2017Uongozi wa Klabu ya Stand United ya mkoani Shinyanga, umeendelea kuwalilia waliokuwa wadhamini wao, Acacia kufuatia kuwaachia mzigo wa deni la shilingi milioni 124 za usajili wa wachezaji wao waliowasainisha msimu uliopita.

Stand imejikuta ikiwa katika hali mbaya kufuatia Acacia kuvunja mkataba katikati ya msimu kulikobabishwa na mgogoro wa kiuongozi ambao ulikuwa umejitokeza katika timu hiyo, hivyo kufanya hali kuwa mbaya kwa wachezaji kutolipwa fedha zao za usajili.

Katibu wa Stand United, Kennedy Nyange, alisema timu yao imepata matatizo katika mechi hizi za mwishoni mwa ligi kutokana na kutokuwa na fedha kufuatia wadhamini wao Acacia kujitoa, hali iliyosababisha kushindwa kuwalipa wachezaji wao mishahara ikiwa ni pamoja na fedha zao za usajili, jumla ikiwa ni shilingi milioni 124.
“Jumla ya wachezaji 13 wanatudai fedha za usajili ambao waliingia mikataba chini ya udhamini wa Acacia, hivyo kumesababisha timu yetu kuyumba kutokana na kushindwa kulipa mishahara wachezaji na kufanya tuhangaike katika kutafuta fedha kunyume na utaratibu, kwani wao walivunja mkataba katikati ya msimu na wao ndio waliotakiwa kuwalipa.

“Jumla ya fedha ambazo tunadaiwa na wachezaji ambazo ni za usajili ni milioni 124, hivyo tunawaomba na kuwasihi waweze kulipa fedha hizo kwa kuwa mikataba ya wachezaji yote tuliingia chini ya udhamini wao na wao ndio wanaopaswa kulipa fedha hizo lakini kila tunapofuatilia imekuwa ngumu, hivyo kusababisha morali ya wachezaji kuzidi kuwa chini na timu kufanya vibaya kwa kuwa wanatudai mishahara ya miezi miwili.


“Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Masele, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga pamoja na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye wote kwa pamoja wameweza kuwafuata Acacia lakini wameonekana kuwa wagumu,” alisema Nyange.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV