April 17, 2017Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe, amedai kuwa wapinzani wao wanaowatuhumu kwamba wanatoa rushwa ili washinde mechi zao, wanakosea sana kutokana na wao kutumia fedha kwa wachezaji wao kwa ajili ya kuongeza morali ya kusaka ushindi.

Hivi karibuni Simba walituhumiwa kutoa rushwa kwa ajili ya kuwarubuni wachezaji wa Mbao FC baada ya kutoka nyuma ya mabao 2-0 na kushinda kwa mabao 3-2 kwenye mechi ya ligi iliyopigwa Uwanja wa Kirumba, Mwanza.

Kutokana na tuhuma hizo za Simba kuwapa rushwa Mbao, viongozi wa Mbao kupitia mwenyekiti wake, Solly Njoshi walimsimamisha kipa wao, Erick Ngwengwe ambaye alidaka kwenye pambano hilo. 

Akizungumza Hans Poppe amesema kwamba wanashangazwa na maneno hayo kutokana na kutokuwa na ukweli wowote, ila yanatokana na wapinzani wao kuchukia aina ya matokeo ambayo waliyapata kwenye mchezo dhidi ya Mbao.

“Tunashangazwa na maneno ambayo wanayasema wapinzani wetu kwamba tunatoa rushwa kwenye mechi zetu ili tupate ushindi zaidi kwenye ule mchezo wa Mbao ambao tulitoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2.

“Kwanza nataka kuwaambia tutoe rushwa ili iweje, maana mechi zote zinachezwa uwanjani, sasa hayo mambo ya rushwa yanaibuka kutoka wapi? Na je, wana ushahidi juu ya ambacho wanakisema?


“Sisi msimu huu fedha zetu tumeziwekeza kwa wachezaji kwa kuwapa fungu la kutosha katika kila mechi kuhakikisha kwamba wanaibuka na ushindi na hakuna jambo lingine kama wao wanavyodai,” alisema Hans Poppe.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV