May 24, 2017


MSUVA NA ABDULRAHMAN MUSA WAKIWANIA MPIRA KATIKA MOJA YA MECHI ZA LIGI KUU BARA WALIZOKUTANA YANGA NA RUVU SHOOTING.

Na Saleh Ally
KATIKA kanuni ya za Ligi Kuu Tanzania Bara, ukiangalia kanuni ya 8 ambayo ni Vikombe na Tuzo, haizungumzi lolote kuhusiana na ufafanuzi wa mfungaji bora kama litatokea suala la kufanana kwa idadi ya mabao ya kufunga kwa wachezaji.

Vipengele vyote 7 katika kipengele hicho cha zawadi, viko kimya na hakuna ufafanuzi katika suala linalopasua vichwa wapenda soka wengi.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Rais wake, Jamal Malinzi limeamua kutumia njia ya mkato au njia ya kuwaridhisha wote, kuanzia wafungaji na timu zao kwa kutoa zawadi ya mfungaji bora kwa kila mmoja wao.

Zawadi ya Sh milioni 5 na ushee imekwenda kwa Abdulrahman Musa wa Ruvu Shooting ambaye mwisho amepambana kuisaidia timu yake kuepuka kuteremka daraja na Simon MSuva ambaye ameisaidia Yanga kubeba ubingwa.

Wote wawili kila mmoja amefunga mabao 14 ya Ligi Kuu Bara. Kwa TFF kama ambacho ameamua Malinzi, kwamba wote ni wafungaji bora wa msimu wa 2016-17.

Hakika mfungaji bora lazima awe mmoja na wanaomfuatia ukianzia yeye, wa pili, wa tatu na kadhalika.

TFF imeamua kuliwahisha hilo suala kwa hofu ya kuzuka kwa mjadala kuhusiana na nani hasa anayestahili kuwa mfungaji bora baada ya Msuva na Abdulrahman kulingana kwa mabao.

Awali, nilipata taarifa kwamba kamati moja iliamua kukaa na kulijadili hilo suala kwa kutumia kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na lile la Afrika (Caf) na kupata mshindi ambaye ni Abdulrahman.

Lakini kutokana na hofu nyingine ya kuzuka kwa mjadala au mzozo na ukizingatia ni kipindi cha uchaguzi, Malinzi akaamua kucheza kama “Pele”. Kwa kulimaliza kwa ‘kubalansi’ mambo.


Huenda zikawa ni hisia za watu, kwa kuwa linakuwa ni jambo dogo sana, lakini sasa litazua mjadala na mwisho uhitimishaji unakwenda kwenye ule mfululizo wa TFF kushindwa kuyafanyia kazi mambo mengi ambayo yametokea katika msimu uliopita kama lile la kadi mbili au tatu za njano za beki Mohamed Fakhi wa Kagera Sugar.


Naweza kusema kweli uchaguzi unakaribia ndiyo maana TFF wanakuwa waoga kwa kila jambo lililo mbele yao na wangependa kumridhisha kila mtu katika kila jambo, kitu ambacho hakiwezekani katika soka.

Kama ungetaka watu wote wafurahi, maana yake katika ligi nzima mechi zote zinazochezwa, matokeo yangekuwa sare halafu sijui mwisho wake ungekuwa upi?

Ukweli kanuni za TFF zina upungufu mkubwa katika suala lililojitokeza sasa na huenda ulikuwa wakati mzuri kwa TFF kukopa kwenye kanuni zinazojitosheleza kama zile za Fifa na Caf.

Baada ya hapo wangetumia vigezo hivyo, halafu wakamtangaza mfungaji bora na baada ya hapo, wakaifanyia marekebisho kanuni yao ya Vikombe na Tuzo ikiwa ni sehemu ya maboresho yanayotokana na mafunzo.

Mfano utaona kanuni za mashindano mengi zinazojitosheleza, wangeangalia mikwaju ya penalti. Katika mabao 14, mwenye penalti chache anakuwa na nafasi ya kuchukua namba ya juu.

Msuva amefunga nne na Abdulrahman amefunga mbili. Kuna kigezo kingine cha dakika alizocheza kwa kuwa hapa inaonyesha Abdulrahman Mussa kacheza mechi zote 30 na dakika ni 2700 na Msuva amecheza 2560.

Pia kuna kuangalia suala la nidhamu, kwamba huyo ana kadi ngapi, yule ngapi na kadhalika. Lakini utaona mpangilio unakuwa na tofauti. Wengine wanaanza na nidhamu wengine wanaanza na penalti au dakika. Inategemea.

Maboresho ya kanuni za uendeshaji pia hutokana na matukio kadhaa kama hili lililojitokeza sasa na TFF Bodi ya Ligi walipaswa kuliangalia kama jambo linalosaidia kuwaamsha na kuleta mabadiliko.
Kuamua “kubalansi” mambo ni kupoteza muda, inawezekana ikawa ni vizuri kwuaridhisha wote lakini mwisho unakuwa si mwendo sahihi kwa mujibu wa mambo sahihi katika jambo linalotaka usahihi.
TFF imeshindwa mambo mengi, haipaswi kushindwa kila jambo hata dogo kama hili. Haishindwi kuonyesha uimara wake wa maamuzi katika jambo fulani.

Hata kama kutakuwa na vigezo baada ya kanuni, basi inapaswa kuviweka wazi na kuweka mambo hadharani kwa kutangaza mshindi mmoja na ingewezekana lililotangazwa na Malinzi lingefuatia kama kuwapa moyo wote wawili kwa kuonyesha juhudi ya kufunga mabao ya kutosha.

Naendelea kuweka msisitizo, TFF inapaswa kuwa imara na kuachana na kufanya mambo kwa ajili ya kuwafurahisha wote kwa hofu yenyewe kuonekana “mbaya” au kutaka kuonekana ni “nzuri” sana. Badala yake itumie kanuni za ligi na vigezo kuhakikisha kila kitu kinakwenda kwa mpangilio sahihi.


Mwisho niwapongeze Abdulrahman na Msuva kwa kuwa wazawa ambao wameongozana katika ufungaji bora wakiwa wamefungana na “kuwatandika” wageni, jambo ambalo tumekuwa tukililia. Kila la kheri zaidi.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic