May 27, 2017Mbao FC kweli imepania kutwaa ubingwa wa Kombe la FA na kubeba zawadi ya Sh milioni 50, kwani kwa siku mbili imekuwa ikitumia muda mwingi wa mazoezi yake kujifunza kupiga penalti.

Leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa, Mbao inacheza na Simba mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba ambapo bingwa wake anapata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mazoezi ya juzi na jana ya Mbao uwanjani hapo chini ya Kocha Etienne Ndayiragije, timu hiyo ilionekana ikitumia muda mrefu kuelekezana kuhusu upigaji wa penalti.

Ndayiragije ambaye ni Mrundi, amesema; “Tunafanya mazoezi ya penalti kwani tunacheza fainali na Simba, lolote laweza kutokea hata tukafika katika penalti.

“Mazoezi haya yatawapa wachezaji wangu uhakika wa kufunga na kutwaa ubingwa hivyo ni lazima niwanoe zaidi katika kupiga penalti.”

Mbao ilikuwa ya kwanza kuwasili Dodoma mapema wiki hii wakati Simba chini ya Kocha Joseph Omog yenyewe iliwasili juzi Alhamisi ikitokea Morogoro ilipoweka kambi ya muda.


Hadi zinafika fainali, Mbao iliitoa Yanga katika nusu fainali ya Kombe la FA kwa kuifunga bao 1-0 wakati Simba iliitoa Azam FC bao 1-0 katika hatua hiyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV