May 27, 2017Na Saleh Ally
UKIUANGALIA msimamo wa Ligi Kuu Bara ulivyo, basi utagundua kuna timu nyingi zinashitakiwa kwa kuwa zimevulunda.

Ziko zilizoteremka na ziko zilizobaki lakini ukweli, msimamo unaonyesha juhudi na uzembe wa kila upande ambao unachangiwa na mambo lukuki yakiwemo yale binafsi.


Achana na timu nne, kama Azam FC, Kagera Sugar, Simba na Yanga ambazo zimeshika nafasi nne za juu. Zilizobaki ni matatizo tupu ambapo ninaamini viongozi wao, wanaona aibu hata kuuangalia msimamo.

Viongozi:
Viongozi wengi wa timu za Ligi Kuu Bara wamekuwa ni watu wanaolenga kufaidika na klabu ambazo wanaziongoza ingawa kuna wengine wamekuwa wakiumizwa na mapenzi yao kwa kulazimika kuchangia hata fedha ambazo zingeweza kusaidia familia zao.

Wale wanaolenga kujinufaisha wana sababu ya matatizo makubwa kwa kuwa wadhamini bado hawana sana imani na mpira nchini. Hivyo kidogo wanachochangia, basi kinapaswa hasa kwenda katika kusaidia.

Viongozi wamekuwa wakitaka kujionyesha mbele ya jamii kama ni watu wenye machungu sana na klabu zao. Lakini malengo ya ndani yanakuwa tofauti na inaonekana wamenuia kujisaidia wao kujulikana au kujifaidisha.

Ulisikia wachezaji wa Ndanda FC wakilia njaa kabla ya mechi moja ya mwisho ya msimu ambayo walitakiwa kushinda! Walifikia kusema walikuwa wakishindia mlo mmoja kwa siku.

Halikuwa jambo jema, lakini mwisho wamefanikiwa kujikomboa wakiwa na njaa. Hivyo kuna kila sababu pia kwa uongozi kutekeleza madai yao.

Tamaa ya baadhi ya viongozi kuamini ndani ya mpira kunalipa sana, imesababisha wao kuingia na hisia za kupata kuliko hata wachezaji, huu ni wizi wa mchana.

MATUMIZI:
Wakati mwingine ni vizuri sana, viongozi wakawa wanajipanga na kuwa na hesabu ya kile wanachokiweza. Lazima kupiga hesabu za matumizi kwa msimu mzima ili kujua mtahitaji kiasi gani.

Hii itawasaidia kujua mapema kama ni kambi kiasi gani, usajili kiasi kipi na mishahara mtalipaje. Maana yake ni hivi, viongozi wawe na matumizi ndani ya uwezo wao badala ya kufikiria “tutajua mbele kwa mbele”.

Mfumo wa mbele kwa mbele ndiyo umekuwa ukichangia mambo kuwa magumu mwishoni na hapo ndipo anapoanza kutafutwa mchawi.

Hesabu za mapema, mipango sahihi tokea mwanzo zinaweza kuwa dawa au gia sahihi ya kumalizia bila ya mikwaruzo mwishoni.

Tena kama inawezekana, klabu zinaweza kuwatumia wataalamu wa mahesabu au watu wa uchumi kuwapangia mipango bora ya msimu mzima na wakaendesha kwa mafungu mawili ya mzunguko wa kwanza na wa pili.

AHADI HEWA:
Mwishoni mwa msimu kumekuwa na rundo la ahadi hewa, wachezaji wengi hasa wa timu ndogo wamekuwa wakiahidiwa kusajiliwa na timu fulani zenye nguvu.

Wakati wa ahadi hizo, nao hutakiwa kufanya uzembe. Mfano kucheza chini ya kiwango ili kuzipa nafasi timu zao za “baadaye” kushinda au kufanya vizuri. Haya mambo yapo ingawa yamekuwa yakifanyika kwa siri kubwa.

Nalenga moja kwa moja kwa wachezaji kwamba wanapaswa kubadilika na kujitambua kwamba, wamekuwa wakifanya upuuzi na wengi wamekutana na ahadi hewa kwa kutumika na mwisho wasisajiliwe.

Wanachotakiwa wao ni kufanya kazi kwa weledi na kuachana na ahadi za kipuuzi za viongozi wajinga wanaowashawishi kufanya ujinga. Wacheze tu na wakumbuke wanaweza kufanikiwa bila kupitia timu kubwa za Tanzania na tuna mifano mingi kama Ayubu Lyanga ambaye amesajiliwa Zanaco ya Zambia akitokea African Sports ya Tanga au Juma Liuzio aliyesajiliwa Zesco bila kuwa staa Ligi Kuu Bara.

AIBU:
Timu za jeshi hasa JKT, imekuwa bingwa wa kupambana kuepuka kuteremka daraja wakati wachezaji wamekuwa wakipata mahitaji karibu yote kwa wakati.

Msimu uliopita ilikuwa kazi kubwa kujikomboa, wanaonekana hawakujifunza lolote, msimu huu wamekuwa wa kwanza kuteremka wakiwa wameshinda mechi tatu tu kati ya 30, yaani 10% tu! Hii ni aibu.

Kuna sababu kubwa ya viongozi kuliangalia hilo, kwanza kujitathmini wao na wanachokifanya. Lakini hata kama ni timu za jeshi, inawezekana zikabadilika na kukaribisha wataalamu zaidi ambao wanahusika na soka.

Inawezekana kuamini kila kitu kinapatikana jeshini, kunaweza kuchangia mdororo wa hizo timu.
Kama zinapata kila kitu, basi bado zinaweza zikasajili wachezaji wakubwa na wenye uwezo. Msimu mmoja tukasikia JKT wamevunja rekodi ya usajili Ligi Kuu Bara.

Si vijana tukisikia Simon Msuva au Ibrahim Ajibu wakiwa JKT na hili linawezekana kama JKT ikiingizwa kwenye mwendo wa malengo ya mabadiliko kwenye mafanikio ya juu zaidi badala ya kuwa timu kama ya kujifurahisha au mazoezi tu, hii inachangia kuwa na kikosi cha “kugombea kuepuka kuteremka daraja” kila msimu.

Toto watoto:
Viongozi wa Toto African ya Mwanza wana maneno mengi sana, lakini kwa vitendo unaweza kusema mengi ni mambo ya kitoto.

Kila mwaka wanagombea kuepuka kuteremka, msimu mwingine pia na mwingine na hawabadiliki.
Wao viongozi wanawatenga mashabiki wengine, wanagombana wao kwa wao na mwisho wanaishia kulalamika tu.

Kila wanapoanza msimu, hadithi yao ni kwamba wamebadilika na huu ni msimu wao. Mwisho wa msimu wanabaki na kazi mbili, kushinda au kuzuia wasifungwe na Simba na kupambana kuepuka kuteremka daraja!

Mwendo wao unatia aibu, msimu mzima walifunga mabao 22 wakafungwa 34! Utaona haikuwa timu yenye malengo tokea mwanzo, mwisho imeingia kwenye dimbwi la kuteremka, ndiyo juhudi zinaanza.

Viongozi wa Toto African walipaswa wote wajitathmini kama wanapaswa kuiongoza. Mwendo wanaokwenda, kitakachofuatia ni kile cha Pamba, kuyumba hadi kupotea. Toto African si ya shirika na inapaswa kuwa ya wananchi wa Mwanza.

Lakini wale ambao ni mashabiki wa Simba wanaoipinga, pia wanapaswa kujitahmini kwamba sasa msimamo wa mwisho, unawasimanga hata wao kuwa “Mwanza ni watu wa manenomaneno tu”.

Shinyanga inakua:
Shinyanga ni moja ya mikoa yenye timu mbili, timu zake zote mbili zimemaliza katika 10 Bora. Hili ni jambo la kujivunia kwao na kama wataendelea hivi, msimu ujao wagombee ubingwa sasa.

Stand United walipoteza wadhamini, lakini mwishoni wamejitahidi. Mwadui FC wameyumba lakini wako katika nafasi ya 10 na inaonekana kama kuna mwendelezo, basi uhakika wa kufanya vizuri msimu ujao upo na bahati nzuri, mashabiki wa mkoa huo ni wapenzi hasa wa soka.

Mbeya maneno pia:
Mbeya City nao wamebadilika, pamoja na kuwa wanapata kila kitu, usajili bora lakini msimamo unawashitaki kwa kuwa wamemaliza katika nafasi ya 11 wakiwa na pointi 33, kati ya watatu walionusurika kuteremka daraja wakiwa na pointi hizo.

Mbeya City imekuwa ikiporomoka tu, ilikuwa kati ya timu zinazowania ubingwa katika msimu wake wa kwanza, ikamaliza nafasi ya tatu, msimu uliofuata ikamaliza nafasi ya nne, msimu uliopita ikaporomoka hadi nafasi ya nane, msimu huu ambao ni wa nne imemaliza nafasi ya 11 ikinusurika kushuka daraja. Isipoangalia, itaporomokea chini.

Viongozi wao pia walianza kutoka kwenye reli baada ya mafanikio kiduchu, ikawa hawashikiki na hakuna kama wao.
Wakaanza vita na vyombo vya habari, wakajivika heshima ambayo hawajafikia, wakaamini wao ni Yanga na Simba na mwisho inaonekana wamepoteza mvuto na mwendo sahihi.

Kama watakuwa waungwana wanaweza kuutumia msimu huu kama funzo kubwa ili warudi katika njia sahihi, la sivyo msimu ujao wataporomoka daraja na kupotea kabisa.

MSIMAMO BARA

                            P       W      D       L        F        A       GD    PTS
1. Yanga               30     21     5       4       57     14     43     68
2. Simba              30     21     5       4       50     17     33     68
3. Kagera             30     15     8       7       33     29     4       53
4. Azam                30     14     10     6       36     20     16     52
5. Mtibwa            30     10     14     6       34     32     2       44
6. Stand               30     9       11     10     25     26     -1      38
7. Ruvu                30     8       12     10     29     33     -4      36
8. Prisons             30     8       11     11     17     24     -7      35
9. Majimaji          30     10     5       15     26     38     -12    35
10. Mwadui          30     10     5       15     32     45     -13    35
11. Mbeya            30     7       12     11     27     32     -5      33
12. Mbao             30     9       6       15     30     38     -8      33
13. Ndanda          30     9       6       15     23     38     -15    33
14. Lyon               30     6       14     10     19     28     -9      32
15. Toto               30     7       8       15     22     34     -12    29
16. JKT                 30     3       14     13     15     29     -14    23

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV