Na Saleh Ally
KAMA wewe ni mpenda soka, lazima utakuwa umewahi kusikia zile tuhuma ambazo amekuwa akisukumiwa Kocha Mecky Maxime wa Kagera Sugar kuwa ni mtu mbaya na amekuwa akipewa hongo ndiyo maana timu anazofundisha hazifanyi vizuri.
Ushahidi wa hilo ni yale mabango ambayo mashabiki wa Kagera Sugar waliingia nayo uwanjani, wakieleza wazi hisia zao kwamba Maxime anapaswa kuondoka. Kama ilivyo kwa baadhi ya waandishi wasiolijua jina lake sahihi, mashabiki hao walitumia Mexime.
Mabango hayo yalikwenda moja kwa moja kuwa Maxime anauza mechi na pamoja na kufanya hivyo amekuwa akiwasingizia wachezaji. Hakuna hata mmoja kati ya hao mashabiki aliyekuwa na uthibitisho kuhusiana na hilo lakini lilikuwa ni shambulizi la moja kwa moja kwa kocha huyo kijana Mtanzania.
Mashabiki mara nyingi hawana huruma, huangalia matakwa yao na kitu cha kwanza kwao huwa ni furaha ya mioyo yao. Inapokosekana, kila mmoja huwa ni adui.
Maxime alionekana hafai kwa kuwa Kagera Sugar ilipoteza mechi yake dhidi ya Yanga baada ya kufungwa mabao 6-2 ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Ilikuwa ni mechi ya 11 ya Kagera Sugar katika msimu na katika mechi 10 zilizopita, Kagera Sugar ilikuwa imeshinda sita, sare tatu na kupoteza mbili dhidi ya Simba na Toto African.
Kufungwa na Yanga, likawa ni kosa kubwa ambalo liliwasahaulisha mashabiki hao ushindi mara sita katika mechi 10. Baada ya mechi dhidi ya Yanga, Kagera Sugar ikapoteza mechi iliyofuata dhidi ya Azam FC kabla ya kushinda dhidi ya Mbao FC na Ruvu Shooting.
Ukiangalia msimamo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara, Kagera Sugar imeshika nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Yanga zilizofungana kwa pointi 68 kila moja.
Azam FC ambayo imekuwa mzoefu wa ‘Top 3’, safari hii imedondoka hadi nafasi ya nne na Kagera Sugar wanafuta ubabe wa timu za Dar es Salaam na Top 3 kama ambavyo Mbeya City imewahi kufanya na kuonekana ni shujaa na kiboko cha vigogo.
Rekodi ya misimu mitano iliyopita inaonyesha Kagera Sugar haijawahi kushika nafasi aliyonayo Maxime msimu uliopita. Maana iko hivi; msimu wa 2011-12, Kagera Sugar ilimaliza katika nafasi ya saba, 2012-13 (nafasi ya nafasi ya 4), 2013-14 (nafasi ya 6), 2014-15 (nafasi ya 6), 2015-16 (nafasi ya 12). Kumbuka huu ni msimu wake wa kwanza Kagera Sugar.
Msimamo unaonyesha baada ya Simba na Yanga zilizoshinda mechi 21 kila moja, Kagera Sugar ndiyo inayofuatia kwa kushinda mechi nyingi zaidi ambazo ni 15. Azam FC ni ya nne baada ya kushinda 14.
Huenda kukawa na hofu, kwamba iwapo Simba itashinda malalamiko iliyopeleka Fifa, maana yake mambo yatabadilika na Kagera Sugar itateremka hadi nafasi ya nne. Azam FC itapanda hadi nafasi ya tatu.
Lakini hii bado haizuii ubora wa Maxime kama kocha uwanjani kwa kuwa kikosi chake kitakuwa kimeonyesha ubora kiufundi na yeye kama kocha ameshindana na presha isiyokuwa na sababu, kutoka kwa mashabiki wenye mihemko na walioshindwa kujiendesha kwa kutafakari mambo kabla ya kujifunza au kufanya ung’amuzi na kupata uhakika.
Wakati fulani niliwahi kusimulia, nilikutana na mashabiki wa Simba wasiojua kufuatilia mambo. Walianza kunizomea na sikujua sababu, lakini sikuwa na hofu kwa kuwa nawajua mashabiki wengi wa soka ni watu wa kukurupuka.
Lakini mwisho, nikagundua kuwa walikuwa wakinizomea kwa kuwa siku moja kabla, Ally Saleh wa Zanzibar alihojiwa na kusema Emmanuel Okwi anapaswa kuwa mchezaji halali wa Yanga na si Simba. Yeye ni wakala anayetambuliwa na Fifa, hivyo alieleza alichoamini.
Hata angekuwa ni Ally Saleh, pia hakupaswa kuzomewa badala yake kama kuna mtu angekuwa ana hoja, angeanzisha. Kuzomea tu kwa maneno ni kutaka sifa usiyostahili na mbaya zaidi unakuwa huna kichwa kizuri cha kujenga hoja.
Waliokuwa wakinizomea wakidhani mimi ni Ally Saleh, walikuwa ni sawa na wale waliokuwa wakimsakama Maxime na mambo ambayo hawana uhakika nayo. Hawajui ukweli uko wapi, ili mradi ni kufuata mkumbo tu na wanakuwa msitari wa mbele kuzomea ili waonekane wajanja.
Kawaida katika makundi ya mashabiki wa soka, wanaopiga kelele sana ndiyo huonekana ni watu wanaojua sana. Kitu kibaya zaidi, wengi wanaotaka kuonekana wanajua sana huwa hawajui mambo na hupenda kupiga kelele tu.
Sasa Maxime anathibitisha mambo kwa vitendo, anakwenda kuchukua nafasi ya tatu akiwa na Kagera Sugar ambayo kushika nafasi kama hiyo hata wengine walikuwa hawajaanza kuishangilia.
Leo Kagera Sugar imemaliza katika nafasi ya tatu, wewe ni shabiki na unakumbuka siku ile ulibeba bango la kumdhihaki kwa maneno makali. Unajisiakiaje leo? Unaendelea kufurahia mafanikio hayo ya Kagera Sugar?
Wewe shabiki, ulisema maneno mabaya dhidi ya Maxime ukitaka aondoke, ukaamini kile ulichoambiwa na mtu aliyeambiwa na yule ambaye hakuwa na uhakika. Leo unajivunia mafanikio hayo?
Vipi mashabiki wanakuwa wepesi kulishwa maneno, wanabugia na kuanza kuyasambaza bila ya kuchunguza. Vipi unakubali kuitwa mtu mzima ambaye kila unachopewa unameza na kuanza “kumwaga” tena ukionekana una jazba kweli utafikiri una uhakika!
Maxime ni mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, mmoja wa manahodha waliofanya vema, waliocheza Taifa Stars na Kili Stars zikiwa na njaa. Hata vipi, bado anastahili heshima yake kama unavyoona mashabiki wa Madrid wanavyoweza kusimama na kumshangilia Xavi Hernandez au Iniesta kwa sababu ya utaifa wa Hispania na ubora wa kazi zao.
Ninaamini kuna watu wengi sana walikata tamaa, huenda leo wangeweza kuwa mbali lakini walikatishwa tamaa na maneno ya mashabiki ambao wengi wanayoyasambaza huwa hawana uhakika na wanachokitoa kwa kuwa hujazwa na wenye malengo yao, nao wakaenda kupayuka tu.
Wengi hawana nia mbaya, lakini hujikuta wakisambaza maneno kwa kuwa tu wangependa kuwa wa kwanza kuonekana katika jamii wanajua jambo fulani. Lakini mara nyingi linakuwa si sahihi.
Wakati fulani, nilikutana na shabiki mmoja wa Simba, hakika alinifurahisha. Badala ya kunilaumu, aliweka hoja mezani. Kwamba “Vipi ulisema Rage alikula fedha ya Okwi na sasa imelipwa?” Mwisho tulimaliza tukiwa tumeelewana kwa kuwa tulikwenda hoja kwa hoja nikimkumbusha kila jambo, mwisho akakubali kwa kuwa nilimpa siku za kufuatilia.
Nilimueleza sikuwahi kuandika Rage kala fedha, badala yake hoja yangu ilikuwa amekurupuka kwa kuwa alipitisha ITC itolewe Simba ikiwa haijalipwa. Alionyesha hakuwa makini na ndiyo maana juhudi za Zacharia Hans Poppe kwenda Fifa zimezikomboa zile fedha. Siku tatu nilizompa akalete maandiko yangu yoyote kuwa Rage kala zile fedha, ziliishia kwenye kile nilichomuambia.
Una hoja, una mawazo? Basi vizuri mueleze mtu kwa njia nzuri na kwa kuwa alichoweka mezani ni hoja, mnaweza kujadili na kupata jambo sahihi.
Maxime amegoma kukatishwa tamaa, makocha wengine hasa wazalendo wajifunze kwake kwamba mashabiki wakati mwingine wanakuwa sumu na kuwasikiliza sana ni kujiondoa katika njia sahihi.
Vizuri kujipima, kama utaona unakosea, basi ukajirekebisha. Kama haukosei basi endelea na kilicho sahihi ili kumaliza na kilicho sahihi. Bravo Maxime.
MSIMAMO
Ligi Kuu Tanzania Bara
P W D L F A PTS
1. Yanga 30 21 5 4 57 14 68
2. Simba 30 21 5 4 50 17 68
3. Kagera 30 15 8 7 33 29 53
4. Azam 30 14 10 6 36 20 52
5. Mtibwa 30 10 14 6 33 32 44
6. Stand 30 9 11 10 25 26 38
MECHI ZA KAGERA LIGI KUU
MZUNGUKO WA KWANZA
Kagera Sugar 0-0 Mbeya City
Kagera Sugar 0-0 Stand United
Kagera sugar 1-0 Mwadui Fc
Ndanda Fc 0-0 Kagera Sugar
Mtibwa Sugar 2-0 Kagera Sugar
African Lyon 0-2 Kagera Sugar
Kagera Sugar 2-0 Prisons
Kagera Sugar 0-2 Toto Africans
Majimaji FC 0-1 Kagera Sugar
Simba 2-0 Kagera Sugar
Jkt ruvu 0-1 Kagera Sugar
Kagera Sugar 2-6 Yanga
Kagera Sugar 2-3 Azam FC
Mbao FC 0-2 Kagera Sugar
Kagera Sugar 3-1 Ruvu Shooting
MZUNGUKO WA PILI
Mbeya 0-0 Kagera
Mwadui 2-1 Kagera
Stand 0-1 Kagera
Kagera 2-0 Ndanda
Kagera 2-1 Lyon
Kagera 2-1 Mtibwa
Prisons 0-0 Kagera
Toto 1-1 Kagera
Kagera 1-0 Majimaji
Kagera 2-1 Simba
Ruvu 1-1 Kagera
Kagera 0-0 JKT Ruvu
Yanga 2-1 Kagera
Kagera 2-1 Mbao
Azam 0-1 Kagera
0 COMMENTS:
Post a Comment