May 29, 2017



Na Saleh Ally
IMEKUWA ni kawaida kwa vyombo vya habari kuwa na ugumu kwelikweli linapofikia suala la kupeana kongole hasa mmoja anapofanya vizuri.

Inapotokea Championi limefanya vizuri, basi itakuwa vigumu kwelikweli kwa Mwanaspoti kuwapongeza kwa kuwa wanajua Championi wanaongoza kwa sasa katika nafasi ambayo walikuwepo.

Ushindani ni jambo la kawaida, nimewatolea mfano Mwanaspoti kwa nia nzuri kabisa nikijaribu kueleza watu wanaoshindana kwamba nao wanaweza kuwapa hongera hata wapinzani wao.

Lakini kuna wale ambao hata si wapinzani, lakini kwa watu wa vyombo vya habari wakisikia Global Publishers wameandaa jambo jema. Hawatakubali kuliripoti kwa kuwa wanaona kama waliofanya hivyo wanafaidika sana.

Wangependa kushangilia au kufurahia au kusifia kitu cha mtu mwingine tu na si cha wanahabari wenzao. Najua Global Publishers walishaamua kujipambanua kwamba wao wangependa pia kupongeza au kukosoa vitu vya wanahabari kwa lengo la kujenga zaidi.

Mimi leo nalenga suala la michuano ya Kombe la Shirikisho ya Azam Sports ambayo juzi umemalizika msimu wa pili na Simba wanakuwa mabingwa wa pili baada ya michuano hiyo kurejea.

Msimu uliopita, mabingwa walikuwa Yanga wakiwatoa shoo Azam FC katika mechi ya fainali huku Simba wakiishia robo fainali kwa “kung’olewa” meno na Coastal Union ambayo haikutegemewa.

Msisimko wa michuano hiyo umekuwa ni wa juu na hakuna ubishi kwa wale waliopata nafasi ya kuona mchezo wa fainali kati ya Simba dhidi ya Mbao FC ya Mwanza, watakubaliana nami kuwa lilikuwa ni bonge la game, kipimo cha soka hapa nyumbani.

Michuano ambayo fainali ziliingia timu tofauti, mgeni wa ligi kubwa na isiyo na historia ndefu dhidi ya vigogo na wanaotisha kwa rekodi kibao, lakini ilikuwa ni patashika nguo kuchanika.

Hakika burudani kama hiyo tuliona katika mechi ya nusu fainali na Coastal Union msimu uliopita au ile ya nusu fainali ya msimu huu kati ya Mbao FC dhidi ya Yanga pale Kirumba jijini Mwanza.

Wanaopaswa kupongezwa sana hapa ni Azam TV ambao wametumia jina la Azam Sports kudhamini michuano hiyo ambayo ina msisimko kweli.

Azam TV ni chombo cha habari, kwa kuwa wana nafasi ya kutoa kiasi cha fedha katika udhamini wamefanya hivyo. Najua siku itafika nasi na wengine tutafuata mfano huo ingawa hapa Championi tumekua tukifanya hivyo kwa michuano ya Uswahilini kwetu na kwa wasomaji wetu.

Kila mmoja hawezi kuwa kama Azam TV lakini anaweza kupita njia yake kusaidia michezo. Hili ni jambo jema ambalo Azam TV wanastahili pongezi kwa kutoa nauli, fedha, kombe na mambo mengine.

Kikubwa ambacho nimeona wanapaswa kuboresha ni suala la zawadi kama itawezekana. Mfano Sh milioni 50 kwa bingwa bila chochote kwa mshindi wa pili.

Ingekuwa wazo langu ningesema bora hata Sh milioni 40 kwa bingwa na Sh milioni 10 kwa mshindi wa pili. Maana unaangalia kwa timu kama Mbao FC walivyopigana pale, halafu wanaondoka bila chochote, hakika si sawa hata kidogo.

Kila jambo huanza taratibu na baada ya hapo unafuatia uboreshaji. Hivyo hakuna ambacho kinashindikana na inawezekana ikafikia michuano hiyo ikazidi kupaa na kuwa bora zaidi kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), litatulia na kuendelea kusimamia vizuri.

Raha ya Azam TV wanaweza kufanya vizuri zaidi kwa kuwa msimu uliopita, walitoa nafasi ya kusikiliza michango na mawazo ya pale walipoyumba. Msimu huu tumeona msisimko zaidi na kama wataboresha zaidi, msimu ujao, huenda msisimko ukawa maradufu. Hongereni sana wadau.



1 COMMENTS:

  1. Azam wamefanya vizuri, issue inakuja kwa TFF wao ndio wanao simamia waweze kurembesha michuano kwa wadhamini zaidi ili ikiwezekana zawadi na pasu kwa timu ziwe za kukidhi.

    Leo hii TFF imekuwa kama inavuta tu mpunga bila kufanya kazi kubwa, sababu tu yeye ni msimamizi wa soka ila swala la kuhimiza maendeleo na usimamizi wa uhakika inakuwa hakuna.

    Timu zinajitahidi ila mazingira hasa ya michezo ni mabaya sana, hasa viwanja, vifaa n.k

    Ukiangalia hata marefa hawana usimamizi wa kueleweka maana utakuta hata jezi zao zimekuwa za hovyo. Wakati TFF wanaweza wakawatafutia wadhamini hao tu marefa wakawa wanatangaza bidhaa za mdhamini ili kupata mchango wa kuwasimamia na kuwa nyanyua...

    Ni mengi sana, ila issue kubwa hapo ni chama cha mpira ndio tatizo

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic