May 29, 2017




Jonas Mkude amejiunga na kikosi cha Taifa Stars, lakini atalazimika kubaki jijini Dar es Salaam kusikilizia afya yake.

Nahodha huyo wa Simba, alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa siku moja baada ya ajali mbaya ya gari iliyotokea Dumila na kuua mtu mmoja.


Mkude alikuwa kati ya waliokuwa katika gari hilo wakitokea mjini Dodoma, kwenda Dar es Salaam.

Kikosi cha wachezaji 21 wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachodhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti, kinatarajiwa kuondoka kesho Jumanne saa 10.45 jioni kwenda Misri.


Taifa Stars ambayo itakuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa kesho saa 7. 45 mchana inakwenda Misri kufanya kambi ya siku nane kujindaa na mchezo dhidi ya Lesotho utakaofanyika Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji hao 21 kutoka hapa Tanzania wataungana na na wengine wawili, Nahodha Mbwana Samatta na Faridi Mussa wanaocheza ughaibuni katika kikosi hicho na kufanya jumla ya wachezaji kuwa 23 watakaokuwa nchini Misri. Tayari Thomas Ulimwengu wa AFC Eskilstuna – Sweden.

Nahodha Msaidizi, Jonas Mkude hatakuwako kwenye msafara huo kutokana na ushauri wa madaktari walioelekeza kwamba nyota huyo wa Simba apate mapumziko ya angalau siku nne.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga ameridhia na kusema kuwa Mkude ataungana na wenzake Juni 8, mwaka huu timu itakaporejea kutoka Misri. Mayanga hajajaza nafasi ya Mkude.

Wachezaji ambao hawatakuwako kwenye kikosi hicho ni pamoja na Haji Mwinyi  (Yanga SC) na Aggrey Morris  (Azam FC) ambao wanaweza kuingia kwenye timu ya Taifa ya Zanzibar baada ya kuwa mwanachama mpya wa CAF kama kocha akiwahitaji.

Mchezo dhidi ya Lesotho ni muhimu kwa Tanzania ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi ‘L’ kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika NCHINI Cameroon.

Mbali ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni Uganda na Cape Verde ambao pia wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa katika mchezo wa kwanza pia kuwania nafasi hiyo.

Kikosi cha Taifa Stars kinachofundishwa na Kocha Salum Mayanga kinaundwana makipa Aishi Manula  (Azam FC), Benno Kakolanya  (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).

Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Kapombe    (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba) na Gadiel Michael.

Walinzi wa kati Erasto Nyoni  (Azam FC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) ilihali viungo wa kuzuia ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude kutoka Simba SC ambaye hatasafiri na timu kwa sasa.

Viungo wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla  (Simba SC) na Mzamiru Yassin (Simba) wakati viungo wa pembeni ni Simon Msuva (Yanga SC), Shizza Kichuya (Simba SC) na Farid Mussa (Teneriffe, Hispania).

Washambuliaji wapo Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Abdurahman Mussa (Ruvu Shooting).

Wasaidizi wa Mayanga katika benchi la ufundi ni Novatus Fulgence ambaye ni kocha msaidizi Patrick Mwangata - kocha wa makipa pia yumo Meneja wa timu, Danny Msangi; Mtunza Vifaa, Ally Ruvu, Daktari wa timu ni Richard Yomba na Daktari wa viungo ni Gilbert Kigadya.


Timu hiyo iliingia kambini Machi 23, 2017 kwenye Hoteli ya Urban Rose, Dar es Salaam kabla ya kesho kwenda Misri na baadaye itarejea Tanzania kucheza na Lesotho, Juni 10, mwaka.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic