May 29, 2017

Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali, amemtaka mshambuliaji wa timu hiyo, Mzimbabwe, Donald Ngoma, asiwayumbishe kwa chochote, na kama amepanga kuondoka kwenye timu hiyo anaweza kufanya hivyo kwani wapo watakaoziba nafasi yake.

Ngoma mwishoni mwa msimu huu, alikuwa na vitendo vya utovu wa nidhamu ndani ya timu hiyo ikiwemo ya kuondoka na kugomea kuichezea timu hiyo kutokana na kutokulipwa mishahara yake.

Ngoma aliyetua Yanga misimu miwili nyuma,  msimu huu alionekana kuwa na msaada kidogo ndani ya timu hiyo kutokana na kutocheza mara kwa mara kwa sababu ya majeraha ya goti ambalo limemfanya akose michezo mingi ya timu hiyo.

Msimu huu Ngoma alifanikiwa kufunga mabao nane, wakati msimu uliopita alifunga mabao 17.

Mzee Akilimali alisema: “Ninachokifahamu ni kwamba, bado ana mkataba na Yanga, ingawa nilimsikia kwamba hana mpango wa kuondoka na nafurahia kuwepo katika timu yetu, lakini kwa haya mambo ambayo anazidi kuyafanya ni vyema akaenda anapotaka.


“Kitu kizuri ni kufuata taratibu na sheria zipo lakini si kuendelea kufanya vitendo viovu, maana hajazuiwa kuondoka kwa sababu yeye siyo wa kwanza kucheza Yanga, tunathamini mchango wake ila ni bora akaenda anapotaka kwani tunaamini wapo watakaoingia kuziba nafasi yake,” alisema Akilimali.  

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV