May 15, 2017Si vibaya ukisema wamekubali kiana!
Maana kipigo cha mabao 2-1 walichokitoa Yanga kwa Mbeya City kinawafanya wabakize ushindi wa mechi moja tu kubeba ubingwa na kesho wanacheza dhidi ya Toto African jijini Dar es Salaam.

Watani wao Simba sasa wanaonekana kukubali kwamba hawana ujanja wa kuwazuia Yanga ambao ni mabingwa watetezi kubeba tena ubingwa.

Kama Yanga wakiutwaa ubingwa msimu huu, maana yake ni kwamba watakuwa wameutwaa kwa mara ya tatu mfululizo, na kuleta tafsiri kwamba wametawala soka la Tanzania kwa sasa.

Yanga ilirejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kuichapa Mbeya City mabao 2-1. Imefikisha pointi 65 sawa na Simba lakini imebakiza michezo miwili wakati Msimbazi wamebakiza mchezo mmoja.

Kwa michezo ambayo Yanga imebakiza dhidi ya Toto na Mbao, hata kama itapoteza mchezo mmojawapo, halafu ikashinda mwingine, na Simba kupewa pointi tatu za mezani ilizopanga kuzifukuzia Fifa, Yanga bado watakuwa mabingwa kwa kuwa wana uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kama kwa vyovyote vile wakilingana pointi, Simba italazimika ishinde mabao kuanzia 11-0 katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Mwadui jijini Dar.

Yanga ambayo juzi Jumamosi iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City, kwa sasa ipo kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 65 sawa na Simba, lakini ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kesho Jumanne, Yanga itacheza na Toto Africans kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, na kama ikiibuka na ushindi, basi itatangaza ubingwa kwani itakuwa imeiacha Simba kwa pointi tatu nyuma, huku timu zote zikibakiwa na mchezo mmojammoja.
Mayanja amesema walikuwa wakisubiri kuona Yanga wakiteleza mbele ya Mbeya City, lakini matokeo ya ushindi waliyoyapata yanawafanya kuamini kwamba wapinzani wao hao wanaenda kuwa mabingwa.

“Tukizungumzia kiufundi na kuacha ushabiki, Yanga wanaenda kuwa mabingwa wapya wa ligi kuu msimu huu kutokana na hali halisi ilivyo.

“Ukiangalia sisi tunashinda, wao wakija pia wanashinda na kukaa juu yetu na wanabebwa na mabao, hivyo kama mpaka mwisho wa ligi ikiwa hivi unadhani nani atakuwa bingwa kama siyo Yanga?

“Kuteleza kwenye mechi kupo, sasa hivi tunasubiri kuona wakipata matokeo angalau ya sare kwenye mechi zao mbili dhidi ya Toto na Ndanda halafu sisi tushinde mchezo wetu wa mwisho, hapo ndiyo tunaweza kuwa mabingwa.

“Lakini hata wakifungwa mechi moja na moja wakishinda, basi mchezo wa mwisho sisi itatulazimu kufunga mabao zaidi ya kumi kitu ambacho ni kigumu sana kutokea, hivyo hatutakuwa na jinsi, acha wawe mabingwa tu,” alisema Mayanja.


Mara ya mwisho kwa Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilikuwa ni msimu wa 2011/12 na hawajashiriki michuano ya kimataifa kwa zaidi ya miaka minne. Hata hivyo, wana nafasi ya kushiriki michuano hiyo safari hii kama watatwaa ubingwa wa Kombe la FA kwa kuifunga Mbao.

1 COMMENTS:

  1. sasa Mayanja naona umeamua kujitoa Imba kwa kuwa hapa Bongo hakunaga desturi ya kusema hayo usemayo, huku kwetu tumezoea kusema "Anabebwa anabebwa" usishangae kumsikia kijana wako Julio akipaza sauti kusema TOTO kauza mechi siku ya kesho hali akijua kuwa anashuka daraja. kimsingi Yanga msitake kusikia maneno ya sifa ya Mayang. kazi bado mnayo kuhakikisha mnashinda mechi zote 2.
    huyu jmhuriJulio yuko wapi??? maana sikusikii kabisaaa, au upo likizo wakati Timu yako Kipenzi inakwenda kutangaza ubingwa???
    Jifunze kunyamaza kwani nalo ni jibu tosha.
    Nawatakia Yanga afya njema na msuva kesho urudi uwanjani umalizie kazi yako ya kutafuta kiatu chako cha dhahabu.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV