May 24, 2017



Hii leo jioni tuzo mbalimbali za Ligi Kuu Bara msimu wa 2016/17, zitatolewa baada ya ligi hiyo kufikia tamati wikiendi iliyopita.

Hata hivyo, Simba inatarajia kutikisa vilivyo safari hii katika tuzo hiyo tofauti na ilivyokuwa katika misimu iliyopita ambapo ilikuwa ikifunikwa na Yanga kila wakati.

Tangu msimu wa 2011/12, mpaka sasa Simba haijawahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora ukilinganisha na Yanga ambayo imechukua tuzo hiyo mara tatu ikifuatiwa na Azam FC mara mbili.

Kutokana na hali hiyo, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ameliambia Championi Jumatano kuwa, safari hii Simba inaweza kuchukua tuzo hiyo kutokana na kuingiza wachezaji wawili katika kinyang’anyiro hicho ambao ni Shiza Kichuya na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ watakaochuana vilivyo na Haruna Niyonzima na Simon Msuva wa Yanga, pamoja na Aishi Manula wa Azam.

Hata hivyo, Maxime alisema anaamini Tshabalala leo hii ndiye atakayeipatia Simba tuzo hiyo kutokana na uwezo mkubwa aliounyesha tangu kuanza kwa msimu huu.

“Nasema hivyo kwa sababu ndiye mchezaji pekee aliyecheza mechi zote za ligi kuu bila ya kukosa hata dakika moja, pia amekuwa akitengeneza nafasi nyingi za kufunga licha ya kucheza nafasi ya ulinzi, hivyo naamini anaweza kuibuka mchezaji bora hii leo,” alisema Maxime ambaye pia anawania tuzo ya kocha bora.

Wachezaji waliyowahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora tangu msimu wa 2011/12 mpaka Msimu wa 2015/16 ni Aggrey Morris (Azam FC), msimu wa 2011/12, Msimu wa 2012/13, alichukua, Kelvin Yondani wa Yanga.

Msimu wa 2013/14, ilitwaliwa na  mshambuliaji wa Azam FC raia wa Ivory Coast, Kipre Tchetche, 2014/15, aliyechukua tuzo hiyo alikuwa ni kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva ambaye kwa sasa pia anawania tuzo hiyo.

Msimu uliopita wa 2015/16, mchezaji bora alikuwa ni  Juma Abdul wa Yanga ambaye msimu huu hayupo kwenye kinyang’anyiro hicho.

Pia leo tuzo nyingine zitakazotolewa ni ile ya Kocha Bora, Mfungaji Bora, Mchezaji Bora wa Kigeni, Mwamuzi Bora, Bao Bora na timu yenye nidhamu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic