June 5, 2017


Baada ya ukimya, Azam FC imeanza rasmi usajili kuimarisha kikosi chake.

Klabu hiyo ya Mbande, imemnasa mshambuliaji anayekuja kwa kasi hivi sasa nchini, Wazir Junior.

Junior aliyependekezwa na Kocha Mkuu Aristica Cioaba, anakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao 2017-18, ambapo alikuwa straika kinara wa Toto African ya Mwanza msimu uliopita, akiwa mfungaji wao bora kwa mabao sita aliyofunga.

Zoezi la kuingia mkataba kwa pande hizo mbili limefanyika leo mchana kwenye Ofisi za Mzizima, zilizopo barabara ya Nyerere, Dar es Salaam, na kusimamiwa na Meneja Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed, aliyekuwa sambamba na viongozi wengine Meneja wa timu, Phillip Alando na Ofisa Habari, Jaffar Idd.

Azam FC ambayo imeanzisha falsafa ya kutengeneza timu ya muda mrefu yenye wachezaji vijana wenye vipaji pamoja na kuwekeza ipasavyo kwenye kituo chake cha kukuza vipaji ‘Azam Academy’ kwa kupandisha wachezaji bora, inaamini ya kuwa ujio wa mshambuliaji huyo utaongeza zaidi makali kwenye eneo la ushambuliaji.

Mshambuliaji huyo anaungana na washambuliaji wengine kikosini, Yahaya Mohammed, Shaaban Idd, Samuel Afful na Yahaya Zaidi, aliyepandishwa kwenye timu kubwa kwa ajili ya msimu ujao akitokea katika kituo cha kukuza vipaji vya ‘Azam Academy’.


Wachezaji wengine ambao tayari wameongezwa kwenye timu kubwa kuelekea msimu ujao wakitokea kituo hicho, ni mabeki Abbas Kapombe, Abdul Haji, Godfrey Elias, kiraka Ramadhan Mohamed na kiungo Stanslaus Ladislaus.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic