June 7, 2017Klabu ya Simba  imepania kufanya makubwa katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kumpandisha ndege kiungo mchezeshaji wa Mbao FC, Pius Busita ili awahi kusaini mkataba.

Busita anacheza namba 8 kwenye kikosi cha Mbao kilichocheza na Simba fainali ya Kombe la FA, mwaka huu na kufungwa mabao 2-1 mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Kiungo huyo, alikuwa mwiba mbele ya kiungo wa Yanga, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Mzimbabwe, Thabani Kamusoko na kiungo wa Simba, Jonas Mkude katika mechi ambazo wamekutana kwenye Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kilicho karibu na Busita, uongozi wa Simba ulimtumia tiketi kiungo huyo Ijumaa iliyopita kwa ajili ya kuwahi kusaini mkataba baada ya kufikia makubaliano mazuri na timu hiyo.

Mtoa taarifa huyo alisema, kiungo huyo mara baada ya kutua jijini Dar es Salaam akitokea nyumbani kwao Mwanza, alikutana na viongozi na Simba huku wakishindwana kufikia makubaliano mazuri katika dau la usajili analolitaka ambalo ni shilingi milioni 30.

"Busita alikuwa huko Dar es Salaam na alikuja kwa ndege baada ya viongozi wa Simba kumtumia tiketi na kikubwa alikuja kusaini mkataba Simba baada ya kufanya mazungumzo ya awali.

"Lakini cha kushangaza amerejea Mwanza bila ya kusaini mkataba na kikubwa walichotofautiana ni dau la usajili ambalo yeye alikuwa akihitaji shilingi milioni 30 lakini uongozi wenyewe wa Simba ulimpa ofa ndogo ya milioni 10 ambazo amezikataa," alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Mratibu wa Mbao, Zephania Nyasi kuzungumzia hilo, alikiri hilo kuwepo na mazungumzo kati ya Busita kwa ajili ya kusaini mkataba na Simba.

"Nikwambie tu hizo taarifa ulizozisikia za kweli kabisa, Busita juzi alikuwepo huko Dar es Salaam na kwa taarifa tulizozipata viongozi wa Simba walimtumia tiketi ya ndege kwa ajili ya kusaini mkataba.

"Lakini amerejea nyumbani juzi Mwanza baada ya kushindwa kufikia muafaka mzuri wa kusaini mkataba na kikubwa ni dau la usajili na wenyewe walikuwa wanataka aingie kambini moja kwa moja kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya SportPesa Super Cup, hivyo wameshindwana amerejea Mbao.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe hivi karibuni alikiri kuwepo mazungumzo na baadhi ya nyota wa Mbao kwa ajili ya kuwasajili kwenye msimu ujao wa ligi kuu akiwemo Mrundi, Yusuph Ndikumana.


"Niseme tu ni kweli kabisa tupo kwenye mazungumzo na baadhi ya wachezaji wa Mbao ambao tumewaona wanafaa kuichezea Simba katika msimu ujao lakini ni siri kwa hivi sasa," alisema Hans Poppe.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV