June 23, 2017



Na Saleh Ally
KUNA mambo mengi sana yanayosababisha timu yetu ya taifa kuyumba kimaendeleo na mara kadhaa tumekuwa tukiyajadili.

Wakati fulani, tulikuwa tukizungumzia kuhusiana na maandalizi duni huku fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya timu ya taifa zikifujwa tu na baadhi ya wahusika.

Lakini kipindi hiki, unaona kuna nafuu kubwa katika maandalizi kwa kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linakwenda kwenye kampeni za uchaguzi mkuu, limekuwa likihakikisha timu ya taifa, Taifa Stars, ina maandalizi mazuri.

Maandalizi yanakuwa mazuri lakini unaona kuna matatizo mengine kadhaa ambayo kwangu ninayaweka hivi. Kocha na wachezaji wenyewe.

Nasema kocha kwa kuwa siamini kama Salum Mayanga anafiti kutufanya kuwa na timu ya ushindani ambayo itatusaidia kufuzu Afcon. Tunahitaji kocha mtaalamu, mwenye uwezo wa kuchukua maamuzi sahihi bila ya woga.

Ninasema hivyo kwa kuwa Mayanga anastahili kuendelea kujifunza na ukweli ni hivi, amepewa nafasi na bado hajaitendea haki na ukweli unaonyesha hatuna muda huo wa kuendelea kufanya mambo kizalendo wakati tunadidimia.

Hivyo kinachopaswa ni kuhakikisha kocha mwingine, mfano Kim Poulsen apewe nafasi ya kuungana na Mayanga kujaribu kupambana kwa mfumo wa “biashara asubuhi”.

Lakini kwa upande wa wachezaji, nafikiri lazima tukubali kwamba tunatakiwa kuwa na watu wenye mawazo tofauti kwa ajili ya kuisaidia timu yetu ya taifa.

Kuwa na wachezaji wengi wanaocheza nje ya Tanzania. Kutaifanya Taifa Stars kuwa na wachezaji waliojifunza na mawazo ya ushindani zaidi na mwisho watakuwa wanajua umuhimu wa kucheza kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika.
Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu na mchezaji mwingine anayecheza hapa nyumbani, hawawezi kuwa na ufahamu sawa nini maana ya Kombe la Mataifa Afrika na unapocheza faida yake ni ipi hasa.

Wachezaji wengi vita yao imekuwa ni kupigana vikumbo kusaini kuzichezea timu za Dar es Salaam. Na kama mchezaji ataipata hiyo nafasi, basi kuondoka inakuwa ni jambo gumu sana kwa kuwa anaona ni kama kupoteza dhahabu. Lakini uhalisia unaonyesha kuishia Yanga na Simba pekee, ni tatizo.

Vizuri kwenda kupata changamoto ambako soka limepiga hatua. Wakati mwingine, taifa likiwa na wachezaji angalau 11 wanaocheza soka la kulipwa, utaona kuna mabadiliko makubwa katika utekelezaji wa malengo kwa kuwa wanakuwa wanaishi na wenye malengo ya juu, maendeleo ya juu na hata changamoto wanazozipata zinakuwa ni zile za kiwango cha juu.

Cape Verde ni nchi ndogo, ni mgawanyiko wa visiwa vidogo kabisa. Huenda ni ndogo hata kuliko mkoa wa Pwani. Lakini leo nao wanacheza Afcon na wanaogopeka. Hii yote kwa kuwa wachezaji wa karibu kikosi kizima wanacheza katika nchi za Ureno na Hispania.

Hili linawezekana kwa Tanzania na wanaotoka kwa sasa lazima wakubali kuanzia nchi za jirani kama ambavyo Ulimwengu na Samatta walivyoanzia DR Congo. Baada ya hapo wanaweza kupata nafasi ya kujitanua Ulaya na kwingineko.

Wachezaji kuona kubaki Dar es Salaam ndiyo mwisho wa ndoto ni ushindi kimaisha ni kujidanganya. Msiishi kwa uoga, msiishi kwa kuhofia kuwaudhi watu wakati mnahitaji kutimiza malengo ya maisha yenu.

Samatta angeona kwenda DR Congo ni kuwakera Simba, leo asingekuwa alipo na wala tusingekuwa tunajivunia kama ilivyo leo.


Kila mmoja anasema; “Samatta ni mfano wa kuigwa.” Sasa mbona hamuigi? Imebaki maneno tu na utekelezaji hakuna! Pekee hawezi kutusaidia tukafika tunapotaka, changamkeni, Dar es Salaam ni kwenu, mtarejea tu.

1 COMMENTS:

  1. Uko sawa kabisa ,hata mini nashangaa sijui ni nani aliye turoga tumkemee

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic