June 28, 2017Aliyekuwa Kocha Mkuu na Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, amesema atashangaa akiona mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma anasaini Simba badala ya kwenda kucheza soka la ushindani Afrika Kusini.

Ngoma ni kati ya wachezaji walio kwenye orodha ya usajili wa Simba katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho.

Simba kama wakifanikiwa kumsajili Ngoma, basi atakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa akitokea Yanga baada ya hivi karibuni kumalizana na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.

Pluijm alisema Ngoma ana ofa nyingi za kwenda kucheza soka Afrika Kusini, hivyo anashangaa kusikia mshambuliaji huyo anakuja kuichezea Simba msimu ujao.

Pluijm alisema, atashangaa kwa kiwango chake alichonacho akiendelea kubaki kucheza soka nchini Tanzania.

Aliongeza kuwa, kwa aina ya uchezaji ya Ngoma, anastahili kucheza Afrika Kusini kwenye soka la kasi, nguvu, stamina na akili katika kupambana na mabeki.

“Hivi ni kweli Ngoma anakuja kusaini mkataba Simba? Kama ni kweli sidhani kama ni sawasawa, lakini ngojea tuone, mimi ninachojua ana ofa nyingi amezipata nchi mbalimbali kati ya hizo ni Afrika Kusini.

“Kwa uwezo na aina yake ya uchezaji, anastahili kucheza soka huko kwani Ligi Kuu ya Afrika Kusini inahitaji wachezaji wa aina ya Ngoma.


“Soka la Afrika Kusini ni la kasi na ushindani, pia inahitaji mchezaji mwenye stamina, pumzi na nguvu za kutosha za kupambana na mabeki hatari,” alisema Pluijm ambaye siku hizi ni kocha wa Singida United iliyopanda daraja msimu huu.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV