June 30, 2017

Na Saleh Ally
HAKUNA anayeweza kukataa kwamba baada ya kuondoka kwa Yusuf Manji, Yanga haijaathirika, hasa kuhusiana na suala la kipato kama klabu kwa ujumla.


Manji alikuwa mwenyekiti, ameamua kustaafu. Lakini tukubaliane kuwa aliwekeza kifedha na kiakili, kwani mipango mingi ya uendeshaji ilitoka kwake na watu wengine wa uongozi wake.

Wakati Manji anakumbukwa lakini lazima tukubaliane kuwa maisha lazima yaendelee kwa Yanga na Wanayanga wote, hivyo lazima kuwe na mipango madhubuti ambayo inanyoosha njia ambayo itakuwa sahihi.

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa kwamba kuhusiana na usajili, Yanga hawako vizuri hasa kuhusiana na suala la kifedha. Wapo viongozi wanaojaribu kutaka kulificha hili, lakini hali halisi haiwezi kufichwa.

Badala ya kutumia nguvu nyingi kutaka kuficha mambo, viongozi wa Yanga wakati wakihangaika na suala la kusaka fedha ili kufanya mambo yaendelee vizuri, basi wana kila sababu ya kupiga hesabu ya mbele.

Hesabu ambayo itawasumbua Yanga inawezekana kabisa isiwe usajili pekee kama ambavyo watu wengi wanaona. Badala yake suala la uendeshaji na hasa baada ya ligi kuanza kwa kuwa hii sasa ni ‘long term plan’, yaani mipango endelevu.

Msimu mzima si kitu kidogo, lazima kuwe na hesabu sahihi ya uendeshaji la sivyo unaweza kukwama njiani. Yanga lazima wawe makini na suala la mishahara kwani wasipoangalia inaweza kuwaangusha.

Kwa mwezi pekee, mishahara ya Yanga inafikia hadi zaidi ya Sh milioni 141, hapa ni wachezaji timu kubwa, vijana, makocha na viongozi. Ukiangalia kwa mwaka mzima, SportPesa ambao ni wadhamini wapya watatoa Sh mlioni 995 kwa msimu wa kwanza.

Misimu mingine minne inayofuatia SportPesa itakuwa inatoa kitita cha Sh bilioni moja. Ukipiga hesabu nzuri unaona fedha za wadhamini zitasaidia mishahara lakini baada ya hapo, Yanga watatakiwa kujitafutia zaidi.

SportPesa wanatoa fedha nyingi sana lakini ukubwa wa mishahara ya wachezaji na viongozi wa Yanga unasababisha ionekane hata fedha wanayopewa ni kidogo sana, jambo ambalo si sahihi.

Kuna kazi kubwa ya kuwapata wadhamini walio tayari kutoa fedha katika kipindi hiki. Hivyo kunatakiwa kuwa na Plan B na viongozi wa Yanga wanatakiwa kujua suala la ubanaji matumizi ikiwezekana kupunguza mishahara mikubwa.

Wachezaji wengi wa kigeni wanalipwa mishahara mikubwa sana, wapo ambao unaona wanastahili lakini bado kunakuwa na suala la kujifunza ili kuhakikisha gharama zinakwenda kama inavyotakiwa ili kuepusha usumbufu wakati ligi itakapokuwa imeanza.

Donald Ngoma ameongeza mkataba na mshahara wa dola 4,000 (zaidi ya Sh milioni 8.8), mshahara kama huo alikuwa analipwa Haruna Niyonzima, sasa analipwa Amissi Tambwe, Vincent Bossou na Obrey Chirwa wakati Thabani Kamusoko analipwa dola 3,500 (zaidi ya Sh milioni 7.7).Utaona kwa mwezi mmoja pekee, kwa wachezaji wachache tu, Yanga inatoa mshahara hadi wa Sh milioni 43, fedha ambazo wanaweza kulipwa timu mbili au tatu za Ligi Kuu Bara kwa wachezaji wote.

Hili suala la uendeshaji na kuangalia mbele ni kubwa zaidi. Kama Yanga itakuwa imewaacha baadhi ya wachezaji wenye mishahara mikubwa ni vema kujihadhari mapema kusajili wenye fedha idadi hiyo.

Lazima kupunguza ukubwa wa fungu la mishahara ili kuwa na uhakika wa mwenendo wa mwanzo hapo baadaye. Si sahihi kwenda kwa kuamini masuala yatajipa huko mbeleni.

Ili kuwa salama, lazima kupanga mipango ya baadaye sasa na kujiepusha na kuingia katika matatizo yatakayokuwa makubwa hapo baadaye. Yanga wasisubiri kesho, wanapaswa kutengeneza njia nzuri ya kupita sasa.

Ukiangalia vizuri, utaona kama Simba walikuwa vizuri sana na makini katika suala hilo. Lakini usajili wao mpya utawafanya mambo yawageukie kama ambavyo unaona Yanga kwa kipindi hiki.

Hauwezi kwa mwezi ukawa na uhakika wa kuingiza Sh milioni 30 au 35 hadi 40, halafu ukawa unalipa mshahara wa zaidi ya Sh milioni 141. Jiulize, pengo la zaidi ya Sh milioni 100 kila mwezi utalizibaje?
Ushabiki au upenzi ni jambo zuri lakini ukitaka kufanya vizuri zaidi, angalia ukweli maana huwa haujifichi.


4 COMMENTS:

 1. Mia arobain na moja milion kwa mwez na kwa mwaka ni bil moja na mia mil mia CTA na kitu. Kwa mwaka hela ya sportpesa ni bil. Sehemu inayoweza kufanyiwa Kaz ni kutafuta wadhamin wengne wasio katika mfumo wa ubashiri. Cdhan kama Yanga wakienda kwenye benk watakosa wadhamin. Pia kuna biashara ya jez tatu kuna viingilio na nne kuliangalia upya suala la haki milik ya matangazo ya TV

  ReplyDelete
 2. Waacheni Yanga wafanye mambo yao kadiri wanavyoona inafaa. Wana mipango yao wewe umekuwa mganga wa kienyeji kutabiri watashindwa kulipa mishahara? Watu wa Simba bhana, mna matatizo kweli. Mmeiandama weee Yanga na mlikuwa mnatamani isifanikiwe hasa wakati huu wa usajili. Sasa baada ya Yanga kufanikiwa kuwabakisha wachezaji wao wote muhimu, mmehamia kwenye jingine.

  ReplyDelete
 3. Sioni shida mimi nitachukua nafasi ya Manji. Mimi naishi America ya Kaskazini. Yanga tutafute wachezaji wazuri hasa safu ya Ushambuliaji. Hakuna mahali tutakapokwama. Mishahara italipwa na kasi yetu Wanayanga itaendelea, daima mbele nyuma mwiko.

  ReplyDelete
 4. Wewe ndio Uwe makini na maandiko yako. You are so biased. Gazeti lako linaandika habari za uongo mtupu. Unajikaanga kwa mafuta yako mwenyewe

  ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV