Na Saleh Ally
KIUNGO mwenye kasi wa Yanga, Simon Happygod Msuva ameondoka Yanga kwenda Morocco kujiunga na Klabu ya Difaa Al Jadid ya nchini humo.
Msuva anakwenda kujiunga na moja ya timu bora za Morocco, timu ambayo ilimaliza msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya pili. Maana yake, msimu ujao itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wakati Msuva anaondoka huenda mashabiki wa soka nchini kila mmoja au kwa makundi atakuwa akiwaza yake.
Lakini cha kwanza ambacho nilikifikiria ni kwamba, Yanga wameingia kwenye mabadiliko na sasa wanaweza kutambua mchezaji anapiga hatua. Achana na wale wapuuzi waliokuwa wakichoma jezi za wachezaji na wengine wakawasifia bila ya kujua pia wanajiingiza katika upuuzi.
Maisha ni hatua, lazima uzipige kubadilisha mambo katika mengi likiwemo suala la maendeleo. Yanga inaingia kwenye rekodi za kuuza mchezaji nchini Morocco, nchi yenye kiwango cha juu zaidi cha soka kuliko hapa nyumbani. Raha zaidi, aliyeuzwa ni mzalendo, hii ni faida kwa timu yetu ya taifa lakini Yanga inafaidika kibiashara.
Biashara:
Nitakuambia Yanga inafaidika vipi kibiashara. Kama Msuva atafanya vizuri, basi kuna nafasi kubwa timu za Morocco, jirani eneo la Afrika Kaskazini au nchi nyingi zilizoendelea kisoka kuanza kuamini Tanzania kuna wachezaji bora zaidi.
Maana yake zitakuja na kwanza zitaanzia Yanga na inawezekana Yanga ikawa imesaidia kuzitangaza timu nyingine za Tanzania nazo zikauza zaidi wachezaji wake nje ya nchi.
Mabadiliko:
Mambo yamebadilika na Yanga inaonyesha ukomavu, leo imefikia inawaachia “key players” tena katika wakati inajiandaa na ligi na michuano ya kimataifa.
Hii inaonyesha hali ya kujiamini na viongozi wako tayari kutafuta mbinu mpya au wachezaji watakaoziba pengo la Msuva na kuwaendeleza wakiisaidia timu na ikiwezekana nao wawe biashara hapo baadaye. Nimpongeze Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga kwa mwendo huu.
Msuva:
Pamoja na kuwapongeza viongozi; binafsi ningependa kumpongeza Msuva na familia yake. Kwa kipindi hiki kuamua kuondoka kwenda sehemu ambayo anajua si maarufu, hajulikani wala hawezi kuwa na thamani kubwa si jambo dogo.
Msuva angebaki Yanga tayari alianza kuwa mfalme, heshima ilikuwa juu na macho ya wengi yalibaki kwake. Lakini amekubali kwenda kuanza mwanzo kama ambavyo Mbwana Samatta aliuvua ufalme wake TP Mazembe na kwenda kuanza upya kabisa KRC Genk.
Nimeandika mara kadhaa kumkumbusha Msuva kwamba anapaswa kuondoka sasa, huu ndiyo wakati wenyewe na hana sababu ya kusubiri kama wengine tumeona, baada ya kufikisha miaka 29 au 30 ndiyo wakafikiri wanafaa kwenda kucheza nje maana walihofia kuuvua ufalme waliokuwa nao kwa wakati husika.
Utaona wapo waliofanikiwa kwenda, mwisho hawakufanya lolote na wengine hata kwenda ilishindikana kwa kuwa umri huo kwa Ulaya, mtu anakwenda kustaafu. Sasa inakuwa kichekesho kucheza soka Tanzania halafu uende ukastaafu Ulaya.
Kuaga:
Pamoja na yote, Msuva kaacha somo kubwa kwa wachezaji wote watakaopata nafasi ya kuhama timu zao. Ameonyesha kweli anatokea katika familia yenye upendo na anaweza kuwa mtu mwenye upendo.
Baada ya kuhakikisha anakwenda Morocco, alikwenda kuwaaga wachezaji wenzake mazoezini, aliwapa mikono na kuwakumbatia baada ya kuwaeleza maneno kadhaa ya kuwatia nguvu na moyo akionyesha upendo wake.
Aliwaaga walimu halikadhalika na kuonyesha ni mtu anayejua anachokifanya na anajua upendo na kuweka akiba ya baadaye. Hilo ni somo kwenu bila ya kujali unachezea Yanga, Simba, Majimaji, Singida United, Azam FC au nyinginezo.
Usisahau, Msuva huyu alikwenda kuaga hadi kanisani kwa kukutana na mchungaji wake akampa jezi naye akamkabidhi biblia.
Familia:
Familia ya Msuva nayo ipongezwe, baba yake mzazi ni shabiki wa Simba wa kutupwa. Alimuunga mkono mwanaye muda wote akiichezea Yanga na kumsisitiza kupata mafanikio kuliko hata muziki ambao Msuva aliamini itakuwa kazi yake.
Wazazi wa Msuva yaani baba na mama yake wanaweza kuwa mfano mzuri sana kwa wazazi wengine kwamba wanaweza wakaiamini michezo, wakawapa sapoti watoto wao na kuwasaidia kufanya vizuri kama ambavyo tumeona kwa Msuva.
Kuamini michezo ni burudani tu yaani si ajira, haina faida ni kuendelea kubaki mzazi mwenye mambo na tabia za kizamani kwa kuwa hutaki kubadilika kwa kujielimisha kwamba sasa si mwaka 1947.
Najua, Msuva atakuwa na kibarua kigumu katika nchi wanayozungumza lugha ngeni zaidi kama Kifaransa na Kiarabu. Aina tofauti ya maisha, mfano vyakula na utamaduni kwa jumla.
Ugumu atakaoupata utakuwa zaidi hata alipokuwa Yanga hadi anakubalika. Kazi ya mwanaume ni kupigana na anatakiwa kupambana hasa kwa kuwa huu ndiyo muda sahihi.
Nimeona anasema anataka kwenda kucheza Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’. Kweli Morocco na Hispania ni karibu kabisa, ni nchi zilizo jirani zimetenganishwa na Bahari ya Mediterranean. Sasa huu ndiyo wakati mwafaka kwa Msuva kuipasua bahari hiyo na kutimiza ndoto zake.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment