July 15, 2017



Na Saleh Ally
SOKA ni burudani hasa na lazima tukubali, inapopatikana nafasi ya kutembelewa na timu kubwa hasa zile zenye wachezaji nyota duniani, kunakuwa na burudani yake.

Katika mechi ya kirafiki kati ya Everton dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, hakika ilikuwa raha. Binafsi nilipata burudani niliyoitegemea pia nikajifunza mengi kama ambavyo nilieleza awali hata kabla ya mechi hiyo.

Nawakumbusha kidogo, niliwaeleza wasomaji namna ambavyo tunaweza kujifunza na kila mmoja akachagua anataka kujifunza nini. Mfano kipa ajifunze, beki, kiungo na fowadi nao wako wa kuwafunza. Makocha hali kadhalika lakini hata ushangiliaji kwa kuwa tulikuwa na wageni kutoka Kenya na England.

Burudani zilikuwa nyingi sana na inaonyesha raha ya kwenda uwanjani. Lakini kati ya burudani hizo, ningependa niiguse ile ambayo shabiki wa Manchester United alipenya hadi uwanjani na kupata nafasi ya kumfikia nyota Wayne Rooney.



Nimeelezwa kijana huyo anaitwa Hassan Omary, mkazi wa Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam ni shabiki wa kutupwa wa Manchester United.

Yeye alifurahishwa kumuona Rooney ambaye ni kipenzi chake wakati akiwa Man United aliyoichezea kwa miaka 13 kabla ya kurejea Everton wiki iliyopita.

Hassan anayependa kujiita Hans Jr, alikatiza ulinzi na kwenda kumkumbatia Rooney kwa nia njema kabisa ya kutimiza matakwa yake. Hakuwa na shida nyingine na baada ya hapo alimuachia na kushangilia, mashabiki wa upande aliotokea nao wakamshangilia kwa nguvu na uwanja mzima ukaunga mkono.



Askari walionyesha weledi, hawakumshambulia kwa kumpiga. Badala yake walimbeba na kumtoa nje ya eneo husika na baadaye niliambiwa aliachiwa.

Lakini pamoja na hivyo, huenda sisi wanadamu ni wasahaulifu. Kwamba mwaka 2010, miezi kama hii, shabiki mwingine alivamia uwanja na kumuwahi Ricardo Kaka, nyota wa timu ya Taifa ya Brazil na kumkumbatia pia.



Hili lilifanyika miaka saba iliyopita lakini hapohapo katika Uwanja wa Taifa. Linaporudia inaonyesha sisi si watu tunaojifunza na hapa ninawagusa baadhi ya askari na wale walinzi maalum wa uwanjani.

Mara kadhaa nimekuwa nikiona mizozo ya hali ya juu kati ya walinzi hao na waandishi. Lakini wananishangaza kushindwa kutimiza majukumu yao kwa kuwa wako busy wakiangalia mpira.

Ninatambua wao ni wanadamu lakini lazima wawajibike kutimiza wajibu wao hasa ulinzi wa wachezaji. Hili liliwahi kutokea basi vizuri lisitokee tena, na hatupaswi kuwa wajinga wa kuamini kwa kuwa makosa yanatokea Ulaya, basi ni lazima tuyahalalishe na kwetu.

Vizuri wanaotoka Ulaya nao wakajifunza mazuri na hasa umakini tokea kwetu badala ya kila baya la Ulaya kuonekana kama likitokea Afrika ni la kawaida tu, ni kutojitambua.



Kama nawaona mkisoma nilichondika, kwanza najua wengi mtanuna. Kama itakuwa hivyo, inakuwa vigumu sana kwenu kujifunza kwa kuwa kila mnachoambiwa hujenga hoja mnashambuliwa au kuhisi ni jambo la kusakamwa. Mkiendelea hivyo, basi matukio kama hayo ya aibu yataendelea.

Kama mnakumbuka wakati shabiki akimvamia Kaka, Rais Jakaya Kikwete alikuwa uwanjani akiwa mgeni rasmi. Juzi shabiki kamvamia Rooney, Makamu wa Rais, mama Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi lakini Kikwete na rais mwingine mstaafu, Ali Hassan Mwinyi walikuwa wageni waalikwa.

Lazima tuwe makini, lazima tujifunze na tukubali kuwa makosa kama hayo yanayoonyesha udhaifu wa ulinzi kwa kuruhusu shabiki anayeruka kutoka jukwaani hadi kumfikia mchezaji katikati ya uwanja hayapaswi kutokea tena na tena na yanapaswa kuwa na mwisho.

Baada ya Hassan kumfikia Rooney, niliona walinzi wa uwanjani na askari wakigeuka kuangalia jukwaani. Najiuliza kwa nini awali hamkufanya hivyo, maana yake mlikubali lile ni kosa na vizuri kulifanyia kazi ili kuepusha maana siku nyingine, anaweza kuingia mtu asiye na nia njema akalipaka matope taifa letu.


1 COMMENTS:

  1. Samahani kwa maelezo yako umeegemea kwenye kuponda ulinzi wetu while mambo haya ni ya kawaida viwanjani na kila siku tunaona hata huko unaposema ugeni wa ulaya yanatokea na ndio maana hata wachezaji wa everton hawakustuka kwani pia imeonesha kuwa rooney anao washabiki hapa nchini kwa mada hii acha kuponda tu kaka haya yanatokea hata nou camp hata vicente calderon hata valderon yanatokea

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic