July 28, 2017
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema usajili wa mshambuliaji, Ibrahimu Ajibu katika kikosi chao wamelamba dume na kusema wapinzani wao Simba wataisoma namba kwa kuwa hakuna asiyejua kiwango cha mchezaji huyo uwanjani.

Ajibu amesajiliwa Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Simba ambapo aligoma kuongeza mkataba mwingine mara baada ya ule wa awali kufikia tamati.

Cannavaro amesema usajili wa Ajibu ni wa kiwango kutokana na uwezo wa mchezaji huyo na kudai kuwa hakuna mtu asiyejua kiwango chake, hivyo wana matumaini makubwa kutoka kwake msimu ujao.

“Usajili uliofanywa na Yanga msimu huu ni mzuri mwalimu amesajili vile alivyotaka yeye kutokana na mapungufu yaliyokuwepo katika kikosi.

“Usajili wa Ajibu ndani ya Yanga ni usajili mzuri kwetu kwani ni mchezaji mzuri na mwenye kipaji cha aina yake na ni mchezaji ninayemuelewa vizuri kutokana na kuuona uwezo wake kwenye ligi na hakuna mtu asiyejua kiwango chake, hivyo ni mchezaj muhimu kwetu wapinzani wasubiri.

“Kuhusu usajili wa Tshishimbi siwezi kumzungumzia kwa kuwa simfahamu na ndiyo kwanza tunakuja kukutana hivyo kadiri tutakavyozoeana ndipo tutajua uwezo wake,” alisema Cannavaro.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV