July 31, 2017



Yule kiungo wa Yanga, Mzambia, Justine Zulu ‘Mkata Umeme’ amepanga kuishitaki timu hiyo katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ili alipwe dola 100,000 (Sh milioni 221) endapo klabu hiyo itaendelea kushikilia msimamo wake wa kutaka kuvunja mkataba wake.

Novemba, mwaka jana, Yanga iliingia mkataba wa mwaka mmoja na Zulu mbele ya wakala wake, Karin Nir raia wa Israel, lakini kwa sasa kiungo huyo anaonekana kukosa nafasi ndani ya timu hiyo baada ya kusajiliwa kwa Mcongo, Kabamba Tshishimbi.

Taarifa tulizonazo zinasema kuwa, bado Zulu hajaungana na timu na yupo kwao Zambia huku Yanga ikiwa na mpango wa kuachana naye ambapo hadi juzi Jumamosi ilikuwa haijamtumia tiketi ya ndege kwa ajili ya kujiunga na timu.

“Zulu bado yupo Zambia, lakini kuna taarifa kwamba Yanga inataka kuachana naye kitu ambacho wakala na mchezaji mwenyewe hawajakubaliana nacho.

“Zulu anataka kurudi Yanga, cha kushangaza uongozi haujamtumia hata tiketi ya ndege huku wakisisitiza kutaka kuvunja naye mkataba. Mkataba wa Zulu na Yanga unamalizika Novemba, mwaka huu.

“Kama Yanga watashikilia msimamo wao huo basi lazima wamlipe dola 100,000, licha ya hivyo bado anawadai zaidi ya milioni 43 zikiwa ni fedha ya mshahara posho na ada yake ya usajili,” kilisema chanzo.

Juhudi za kumtafuta Zulu kutaka kuzungumzia ishu hiyo, hakupatikana, lakini wakala wake ambaye ni Karin, alisema: “Naiheshimu Yanga na naipenda. Tulijaribu kufanya makubaliano lakini ikashindikana. Wanatakiwa kuheshimu mkataba kama sisi tunavyowaheshimu. Tunawapa muda mpaka kesho (leo) Jumatatu ambapo dirisha la usajili Zambia linafungwa, hii ishu iwe imeeleweka la sivyo tunakwenda kuwashtaki Fifa.”

Walipotafutwa viongozi wa Yanga kuanzia na katibu mkuu wa klabu hiyo, Charles Mkwasa, aliomba atafutwe leo Jumatatu ili aweze kulitolea ufafanuzi wa kutosha lakini alipopatikana mwenyekiti wa kamati ya usajili, Hussein  Nyika, alisema: 


“Huo ni uongo wao, tunachofahamu ni kwamba Zulu anakuja kuungana na wenzake, hatuna mpango wa kuachana naye."

SOURCE: CHAMPIONI 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic