July 17, 2017



Na Saleh Ally
HATUWEZI kusema kila jambo alilofanya aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi lilikuwa ni baya au baya kupindukia.

Mara kadhaa nimesema wazi kwamba kuna sehemu alijitahidi lakini ni chache sana ambazo nyingi niliamini zilipaswa kukemewa.

Lakini zile chache alizofanya hata kama aliziendeleza, basi zilipaswa kupongezwa kwa kuwa kama unataka kuwa mwanadamu bora, unapokosoa vizuri pia na kusifia.

Sehemu chache kama suala la vijana ambalo alilikuta likiwa limeanza lakini halina kasi, aliliendeleza vizuri ingawa mwanzo alianza na makosa makubwa.

Inawezekana kabisa suala la washauri wake wengi kutokuwa na uzoefu au kutojua mambo mengi ya soka walifanya aende kombo kama ile ishu ya Taifa Stars Maboreshoambayo ilifanyika Tanzania pekee duniani kote na hakuna cha kuficha, ilifeli na waliokuwa wadhamini wakati huo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), walilalamika kwamba haikuwa na faida.

Baadaye, kwa kuwa wapo walioweza kumkosoa Malinzi bila ya woga, aliona haya na alibadilisha baadhi ya mambo na kwa vijana kuna mambo alifanya vizuri na nilimpongeza sana.

Lakini katika mengine mengi sana alifeli tena kwa kiwango cha juu kabisa. Angalia namna utendaji ulivyokuwa duni na matumizi ya fedha pia yalikuwa duni na nilianza kuandika ripoti ya ukaguzi wa matumizi ya fedha kitambo.

Ilionyesha walakini mkubwa. Malalamiko kuanzia ndani ya TFF hadi nje. Angalia kamati alizoziteua kwa ajili ya maamuzi mbalimbali ya soka zilikuwa na maamuzi duni yaliyoonyesha kujaa ushabiki na kutaka kufurahisha baadhi ya watu fulani.

Yalikuwa ni maamuzi ya kibabe, hakukuwa na woga wa unyang’anyi wa haki. Mara zote nilieleza kuhusiana na uduni na ubovu wa kamati hizo. Najua hamkunisikiliza, lakini cha mlilia haki mwisho huzaa haki, na mwisho unaona kamati hizo duni zote zilisambaratishwa na kubadilishwa au kufanyiwa marekebisho makubwa kabisa.

Hii ilidhibitisha kile ambacho nilikililia marazote na kueleza kwamba haikuwa sahihi. Nashangazwa na wote mliofumba macho kutaka kuonyesha hakukuwa na upungufu kutokana na matakwa yenu binafsi, furaha zenu au shukurani kwa misaada mliyopewa au furaha mliyopewa huku mkiona mpira wa Tanzania unadidimia.

Sasa Malinzi hayupo na uchaguzi utafanyika Agosti 12,mwaka huu mjini Dodoma. Kamati ya uchaguzi imebadilishwa pia baada ya ile iliyokuwepo kushadadia madudu kama yaliyokuwa ndani ya TFF kwa miaka yote.

Tutayaacha ya Malinzi tutakuja kuyazungumza baadaye. Naamini siku itafika wakati tukiweka kila kitu wazi lakini sasa hayupo na macho yetu kwenu mnaogombea.

Sioni mtu mpya sana katika wagombea wa Urais wa TFF, ukiachana na Ally Mayay au Shija Richard ambao wao ninaweza kuhoji kuhusiana na uzoefu wao.

Waliobaki hata nafasi ya umakamu wa rais, asilimia 95 waliongoza TFF katika ngazi tofauti. Sasa wanakuja na nini, wanataka kuchukua tu nafasi kwa ajili ya heshima au wana kitu.

Niliwahi kuandika kumuelezea Mayay kwamba vizuri wakazungumzia suala la sera na kipi walichonacho kwa ajili ya kuung’oa mpira topeni. Si kusema tu turudishieni mpira wetu na ndiyo iwe sera. Wako walionielewa na wengine walilalamika sana, sikujali kwa kuwa hawakuwa na hoja za msingi na nilijua ujumbe uliwafikia hadi ndani ya mioyo yao na wataufanyia kazi.

Makosa mengi yaliyofanywa kipindi cha Malinzi vizuri yasirudie na natoa ushauri wanaotaka kugombea wajue TFF ni ya Watanzania na si wao wanaotaka kugombea.

Wajue wanaingia kuwa watumishi wa watu na si nafsi zao. Wajue wanaingia kupigania maendeleo ya soka ya Tanzania na Watanzania wenyewe na sio familia zao.


Kama unaona unataka kugombea ili kusaidia kubadili maisha yako kwa fedha za udhamini wa wadhamini wa TFF,kaa kando mapema, usije kutulaumu baadaye.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic