July 5, 2017


Na Saleh Ally
Baada ya Taifa Stars kufanikiwa kutinga nusu fainali ya Kombe la Cosafa, watu wengi walianza kuwazodoa wale waliokuwa wakimkosoa Kocha Salum Mayanga.

Wengi waliamini Mayanga sasa ni bora kabisa huku wakiwaona wale ambao wamekuwa wakimkosoa kama watu wabaya.

Mimi naanza kuwa wa kwanza kuendelea kusema kwamba Mayanga ni kocha anayejitahidi lakini kwa kiwango chake sidhani kama tuna nafasi ya kufika mbali.

Michuano ya Cosafa inaweza kuwa sehemu ya mazoezi mazuri kwa Taifa Stars kujiandaa kwa michuano ambayo tunaihitaji.

Cosafa ni sehemu ya mazoezi kwa kuwa wote tunajua malengo yetu ni michuano mikubwa mitatu ya Afrika. Yaani ile ambayo inahusisha wachezaji wa ndani ya bara la Afrika maarufu kama Chan na ile ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).


Michuano ya tatu tunayotaka mafanikio na tunaweza kuitumia kama njia sahihi ni Kombe la Dunia, wote tunalijua hili.

Hivyo lazima tuone na tujipime, hakika kuanza kujipima kwa Cosafa na kuona Mayanga anaweza kila kitu kwangu napingana nanyi kweupe bila ya kujali.

Taifa Stars ni timu yetu, tuna haki ya kuikosoa na kuisifia tena bila ya woga. Waliokosoa huenda walitoa changamoto ambayo imechangia Mayanga kuendelea kujituma na kufanya vema.

Mayanga ni kocha mzalendo na tunapaswa kumuunga mkono na mimi namtia moyo kwamba aendelee kufanya kazi zake kwa kujituma.

Kweli Mayanga ana nia nzuri lakini tukubali uzoefu na utalaamu wake, kwa ushindani dhidi ya Cape Verde na Uganda bado kuna kazi ngumu sana. Basi ikiwezekana aongezewe nguvu lakini tusipakane mafuta kwa mgongo wa chupa.


Lakini hatuwezi kumdanganya kwa kuwa eti ni mzalendo. Ninachoona kama tutaendelea kujaribu hivi kwa hofu ya gharama au kutaka kufanya mambo kwa kivuli cha uzalendo, basi tutaendelea kukwama.

1 COMMENTS:

  1. UKO SAWA KABISA TATIZO LETU KAMA WA TANZANIA HUWA HATUPENDI KUAMBIWA UKWELI

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV