July 5, 2017

UWANJA WA KAUNDA-YANGA


Na Saleh Ally
FURAHA ya mashabiki wa soka hasa wa klabu za Yanga na Simba, ni kuona klabu zao zinafanya usajili wa kukata na shoka wa wachezaji wapya.


Ikitokea mchezaji fulani akajiunga na timu nyingine akiwa anatokea kwao, basi ujue atakuwa ni adui mkubwa kwa kuwa wangependa abaki na hasa wanayemtegemea.


Kama pia itatokea mchezaji ilielezwa atakwenda Simba, lakini uongozi wa klabu yao mfano Yanga ukafanya juhudi za ziada kuhakikisha unambakiza, basi watachukia sana, hasa kama kuna chombo cha habari kilisema ameishamalizana na upande wa pili.


Wao hawatajali hata kama ilielezwa hakuwa amesaini lakini amemalizana na kukubaliana nao. Wala hawawezi kufurahia au kushukuru kwamba kujulikana kwa kilichotokea upande wa pili hulisaidia jambo kwao kuamka na kufanya kila linalowezekana kumbakiza mchezaji fulani.


Furaha ya mashabiki hasa kwa kipindi hiki inaonekana ni usajili na wakisikia nyota fulani amebaki au nyota fulani wanayempenda amesaini, hiyo ni faraja.

UWANJA WA SIMBA BUNJU


Kama mashabiki wana furaha, basi uongozi utaonekana unafanya kazi kubwa sana na wenyewe hauwezi tena kuwa katika presha kwa kuwa unaowatumikia hauna tofauti nao na umewafurahisha.

Ajabu, katika mashabiki wao hakuna anayehoji kuhusiana na uwanja. Kwamba hata hao wachezaji wapya wanaosajiliwa kwa mamilioni, vipi usimaliziwe uwanja?


Yanga wana uwanja upo makao makuu ya klabu yao pale Kaunda. Lakini ni uwanja tu na si uwanja wa mazoezi. Kama utafanyiwa ukarabati, basi utaweza kuwa tayari kufanyiwa mazoezi.

Simba wana uwanja na wana nyasi bandia tayari. Kinachotakiwa ni suala la ujenzi tu. Sasa vipi nao hawaumalizii ili kuepusha maajabu ya kuendelea kuwa klabu kubwa isiyokuwa hata na uwanja wa mazoezi miaka nenda rudi?

Mashabiki hawafurahii uwanja, wanafurahia wachezaji wapya au nyota wao kubaki. Lakini viongozi wanaweza kuwa chachu na kubadilisha mawazo ya wanachama kwamba uwanja ni muhimu sana.


Kwa fedha walizotumia Simba kwa usajili, kama wangetumia nusu yake kumalizia uwanja mambo yangekuwa safi kwao. Hii pia ingeweza kufanyika kwa Yanga ili kuhakikisha wana sehemu ya mazoezi.

Yanga na Simba hadi sasa kutegemea viwanja vya shule na vile vya Jeshi la Polisi si sawa. Viongozi, onyesheni nanyi ni wapya badala ya kuwa “Mvinyo wa zamani katika chupa mpya.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic